KANUNI za Ligi Kuu Tanzania Bara zimemuondoa kwenye benchi kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi kwenye mchezo wa watani wa jadi, Simba na Yanga wa Aprili 30. Lakini amesisitiza kwamba kipigo na kasi yao itakuwa palepale.
Yanga itakuwa mwenyeji wa mchezo huo wa mzunguko wa pili wa Ligi bila kocha wake mkuu ambaye juzi aliondolewa kwenye benchi kwa kadi nyekundu katika mchezo wa robo fainali na Geita wa Kombe la Shirikisho (ASFC), ambao timu hiyo ilishinda kwa penalti.
Adhabu hiyo inamuondoa Nabi kwenye benchi katika mechi tatu, kwa mujibu wa kanuni za Ligi Kuu ambazo pia zinatumika kwenye ASFC.
Kanuni ya 2.11 inasema kocha atakayetolewa kwa kadi nyekundu na mwamuzi kwenye mchezo wa Ligi Kuu atafungiwa kuongoza timu yake kwenye vyumba vya kuvalia na benchi la ufundi katika mitatu inayofuata ya timu yake na kutozwa faini ya Sh500,000.
Yanga ikishinda itaongeza tofauti ya pointi 13 na Simba ambayo itasubiri Yanga ipoteze michezo minne na kupata sare moja kwenye mechi 10 itakazokuwa imebakisha wakati huo Simba ikishinda idadi kama hiyo ya mechi ili ziende sawa.
Akiuzungumzia mchezo huo, Nabi alisema si tatizo kutokuwepo kwenye benchi katika mchezo huo si tatizo kubwa kwa kuwa hata angekuwepo kwenye benchi, asingeingia uwanjani kucheza.
“Licha ya kutokuwepo kwenye benchi, lakini majukumu yangu kama kocha nitayatimiza nikiwa nje ya eneo hilo na timu ikafanya vizuri na kuondoka na pointi tatu.Nitawaandaa wachezaji wangu kuifunga Simba bila uwepo wangu kwenye benchi katika mchezo huo,” alisema kocha Nabi ambaye majukumu yake sasa yatafanywa na wasaidizi wake wakiongozwa na Cedric Kaze aliyewahi kuwa kocha mkuu wa Yanga. Rekodi zinaonyesha Kaze kutowahi kufungwa na Simba.
Kaze akiwa kocha mkuu, aliiongoza Yanga katika mechi mbili dhidi ya Simba, na kupata sare ya bao 1-1 kwenye ligi na kuichapa mabao 4-3 kwa penalti na kuchukua ubingwa wa kombe la Mapinduzi Zanzibar.
Akizungumzia maandalizi ya kikosi chake, Nabi alisema amewapa wachezaji mapumziko ya siku tatu mpaka nne ili kupata muda wa kupooza mwili na kuwa sawa kurudi katika hamu ya kufanya mazoezi ya kutosha.
“Tutakuwa na siku si chini ya kumi kufanya mazoezi na maandalizi mengine muhimu ya kutosha kulingana na vile ambavyo Simba walivyo na bahati nzuri tutaendelea kuwaona wakicheza,”
Alisema akiwa jukwaani, anaamini wachezaji wake watacheza kwa maelekezo na yeye akiendelea kuwasiliana na wasaidizi wake kwa karibu kuhakikisha wanashinda mchezo huo.
“Benchi la ufundi ataliongoza, Cedrick Kaze nitampatia maelekezo kabla ya mechi na tutakuwa tukiwasiliana wakati mchezo unaendelea na kuona namna gani tunashinda dhidi ya Simba ili kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa msimu huu.”
Kocha huyo alieleza tukio la yeye kupewa kadi hiyo kuwa ni baada ya kuhoji kwa mwamuzi msaidizi kwa nini zimeongezwa dakika tano na hazikutumika.