Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli ameweka wazi kuwa nguvu kubwa kwa sasa ni kuelekea mchezo wao wa watani wa jadi dhidi ya Simba unaotarajiwa kuchezwa Aprili 30,Uwanja wa Mkapa.
Mchezo huo utakuwa ni wa mzunguko wa pili baada ya ule wa mzunguko wa kwanza ubao wa Uwanja wa Mkapa kusoma Simba 0-0 Yanga.
Bumbuli amesema kuwa kasi yao ipo palepale na hawana mashaka kwa mechi zao zote zijazo ikiwa ni pamoja na mchezo dhidi ya Simba.
“Tunahitaji kushinda kwenye mchezo wetu wa ligi ujao dhidi ya Simba kwa kuwa tunahitaji pointi tatu zao ambazo ni muhimu kwetu na tunakwenda kufanya maandalizi mazuri.
“Ukweli ni kwamba ushindani ni mkubwa hilo tunalijua lakini tupo kwa ajili ya kufanya vizuri hasa kutokana na uimara wa kikosi ambacho tupo nacho kwenye mechi zetu ambazo tunazicheza,mashabiki wajipange waje kwa wingi kuona burudani,” amesema Bumbuli.
Siku 16 zimebaki kabla ya mchezo huo kuchezwa huku Yanga ikiwa ni namba moja kwenye msimamo na pointi zao ni 51 huku Simba ikiwa na pointi 41 zote zimecheza mechi 19.