Kiungo wa zamani wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC na Timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ Amri Kiemba amekuwa sehemu ya wadau wa Soka la Bongo waliothubutu kuwatia moyo wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, hasa wanapokua nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Amri Kiemba amejitokeza hadharani na kuwa sehemu ya Wadau wa Soka la Bongo walioonesha Uzalendo kwa kuandika maneno matamu kuelekea mchezo wa Mkondo wa Kwanza Hatua ya Robo Fainali utakaopigwa Kesho kutwa Jumapili (April 17), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Kiemba anaamini Simba SC kushinda michezo yake ya nyumbani liemkua jambo la kawaida kwa sasa, japo linachukuliwa kama hujuma kwa baadhi ya watu wasiopenda mafanikio ya klabu hiyo, ambayo imetinga Robo Fainali katika michuano ya CAF mara tatu ndani ya miaka minne.
Ameandika Simba SC kufanikisha azma ya kushinda nyumbani sio jambo baya na linapaswa kupewa heshima kubwa kwa klabu za Bongo, lakini akawataka Viongozi, Wachezaji, Wanachama na Mashabiki kuzipuuza Propaganda zinazopikwa kwa sasa na waendelee kuamini Silaha ya maangamizi ni Uwanja wa Mkapa.
Amri Kiemba ameandika: Sio dhambi Simba kushinda mechi za nyumbani pekee kwenye michuano ya Africa kutokana na mifumo ya usimamizi wa mchezo wenyewe kutoa faida zaidi kwa mwenyeji ndio maana mgeni akapewa faida ya goli la ugenini.
Imewachukua UEFA miaka mingi kurekebisha usimamizi wa michezo yao na kujiridhisha kunakuwepo na usawa wa ushindani ndani ya kiwanja kwa asilimia kubwa ndipo umeona wameondoa faida ya goli la ugenini.
Kwa wale ambao hawajawahi kushiriki michuano ya Africa ni rahisi kushambulia mikakati ya timu kujipanga kiakili kuhakikisha mechi za nyumbani yanapatikana matokeo chanya na kuisaidia timu kuendelea mbele kwenye michuano husika.
Michuano ya Africa ni tofauti na mnavyoijadili vijiweni inahitaji kuwa na timu imara ndani ya kiwanja lakini pia timu bora na bobezi kupambana nje ya uwanja kwa kutengeneza mazingira rafiki kwa timu kushindana na kupata matokeo kwani ndio utaratibu wa michuano ili kama timu inafungwa basi mjadala uwe ni kuboresha kikosi na sio tumehujumiwa.
Kama utaamini kwamba benchi la ufundi linatosha kuiandaa timu kushindana ndani ya kiwanja inatosha kwenye michuano ya Africa utaendelea kufukuza waalimu na kufanya usajili kila msimu hivyo basi bila kupepesa kama unataka kushindana Africa inakupasa kushindana kwa namna wanavyoshindana tengeneza timu bora ndani ya uwanja na timu bora nje ya uwanja.
Kwa hili niwapongeze Simba SC kwa kuanza kushindana namna ambavyo tulipaswa kushindana toka awali ndio maana kutokana na ukomavu huo hatusikii tena wakilalamika juu ya hujuma kwenye michuano
Hizi propaganda zinazoendelea ni khofu ya timu pinzani ya kucheza na Simba Kwa Mkapa kwani wanajua ugumu wa kupata matokeo uwanjani hapo na baadhi ya watanzania wamelibeba kama agender kuhakikisha wageni wanacheza kama wako nyumbani na sio ugenini inafikirisha.
Wakati mwingine badala ya kutaka watu wote waliokuzunguka wasiwenacho kama wewe unapaswa kufikiria ni nani utamuomba msaada ukikwama kwa maana hiyo tunapaswa kujivunia mafanikio ya Simba kama nchi kwani sasa hivi tunaanza kuzoea kupeleka timu nne .
Kila la kheri Simba, kila la kheri Tanzania
Makala haya yaliandikwa na Amri Kiemba.