Home Habari za michezo PSG WAPANGA KUTUMIA NJIA TATU ‘KONKI’ ZA KUMZUIA MBAPPE KUSEPA…NEYMAR KUPIGWA BEI…

PSG WAPANGA KUTUMIA NJIA TATU ‘KONKI’ ZA KUMZUIA MBAPPE KUSEPA…NEYMAR KUPIGWA BEI…


Oparesheni bakiza Mbappe. Waweza kuiita hivyo baada ya Paris Saint-Germain kuja na mpango mathubuti waliougawanya kwenye makundi matatu ili kuhakikisha Kylian Mbappe abakizwe na haondoki kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi huko Ulaya.

Vinara hao wa Ligue 1 wanajiandaa kumpoteza Mbappe, 23, bure kabisa mwishoni mwa msimu huu kutokana na mkataba wake kufika tamati huko Parc des Princes.

Kwa muda mrefu amekuwa akihusishwa na Real Madrid na huko Bernabeu ndiko anakoonekana kwamba anakwenda kucheza ndani ya miezi michache ijayo. Lakini, PSG bado hawajakata tamaa ya kushindwa kumsainisha dili jipya ili abaki.

Na kwa mujibu wa Le Parisien, klabu hiyo imekuja na mpango wa njia tatu za kuhakikisha mshindi wao huyo wa Kombe la Dunia haondoki na anaendelea kubaki kwenye kikosi chao kwa miaka mingi zaidi.

Mpango wa kwanza, wazo linaloshtua ni kumuuza Neymar. Mabosi wa PSG wanaamini kwa kumchezesha Lionel Messi chini kidogo kutamruhusu Mbappe kuwa na uhuru kwenye eneo la kushambulia na hilo linaweza kumshawishi akaamua kubaki.

Neymar na Mbappe walijiunga na PSG mwaka 2017 – ambapo staa wa Brazil alitokea Barcelona na Mfaransa Monaco.

Mpango wa pili wa PSG katika kumbakiza Mbappe ni kusajili wachezaji wengine wapya. Mabosi wa Parc des Princes wanaamini wanaweza kumshawishi Mbappe akabaki kwenye timu hiyo kama watamwongezea wachezaji wenzake ambao wamekuwa akicheza nao kwa mafanikio makubwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Ufaransa. PSG imelenga kuwasajili viungo, Aurelien Tchouameni wa Monaco na Paul Pogba wa Manchester United.

Mpango wa tatu wa PSG kumbakiza Mbappe kwenye kikosi chao ni kumpa mshambuliaji huyo unahodha. Beki wa kati, Marquinhos kwa sasa ndiye nahodha wa timu hiyo, licha ya kwamba Mbappe alipewa kitambaa cha unahodha kwenye mechi yao ya ushindi wa mabao 6-1 dhidi ya Clermont hivi karibuni.

Staa huyo amefunga mabao 164 katika mechi 211 alizochezea PSG, ikijumuisha mabao 32 katika mechi 40 alizocheza msimu huu. Kikosi hicho kinachonolewa na kocha Mauricio Pochettino kipo vizuri kwenye msimamo wa Ligue 1 kikiongoza kwa tofauti ya pointi 15 dhidi ya timu inayoshika nafasi ya pili Marseille na kuna mechi sita tu zimebaki.

SOMA NA HII  FAINALI YA LIGI YA MABINGWA ULAYA YAWEZA KUPIGWA WEMBLEY

Lakini, kuhusu taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya watalazimika kusubiri walau kwa miezi 12 mingine baada ya msimu huu kukomea kwenye hatua ya 16 bora kwa kuchapwa na Real Madrid.