Kama utani Geita Gold wametua tano bora kwenye msimamo wa Ligi Kuu baada ya kuendelea kufanya vizuri kwenye mechi zao na kuvuna pointi ambazo zinazidi kuwaweka pazuri katika mbio za kumaliza kwenye nafasi muhimu na kuzoa bonasi mbalimbali kutoka kwa wadhamini wa ligi hiyo.
Juzi timu hiyo iliendeleza wimbi la ushindi kwenye uwanja wa Nyankumbu mjini Geita ikiitandika KMC mabao 2-0 yakifungwa na Amosi Kadikilo dakika ya 48 na George Mpole dakika ya 75 na kuipaisha hadi nafasi ya tano kutoka ya tisa wakivuna pointi 27 huku KMC ikiangukia kwenye nafasi ya tisa na alama zao 24.
Bao alilofunga George Mpole katika mchezo huo ni la 10 msimu huu akilingana na Reliant Lusajo wa Namungo wakiwa nyuma ya Mkongomani wa Yanga, Firston Mayele aliyetikisa nyavu mara 12.
Akizungumzia ushindi huo, Kocha Msaidizi wa wachimba dhahabu hao, Mathias Wandiba ‘Masta’ alisema sasa wanapambana ili kuifunga Azam mechi ijayo na wachezaji wanatambua majukumu yao.
“Tulipata plani nzuri tumepata utulivu tukiwa nyumbani ndiyo siri kubwa iliyotubeba kupata matokeo ya leo kwasababu tuliwasoma vizuri KMC walitufunga mechi ya kwanza na leo tumelipa kisasi ilikuwa lazima tupate pointi tatu na kulipa zile goli mbili,” alisema Wandiba.
Kuelekea mchezo wa Ijumaa dhidi ya Azam ukipigwa uwanja wa Nyankumbu FC,Wandiba alisema wanaiheshimu Azam ambayo ni kubwa na nzuri lakini wamejiandaa kupata ushindi nyumbani kwa kuandaa mbinu bora zitakazowapa matokeo ya kushtua.
“Malengo ya sasa ni kwa Azam tunafahamu ni timu kubwa na nzuri lakini tunajiandaa kwenda kupata matokeo katika uwanja wetu wa nyumbani hakuna namna nyingine yoyote,” alisema Wandiba.
Kocha Msaidizi wa KMC, Ahmad Ally, alisema wamepoteza mechi dhidi ya Geita Gold kutokana na beki zake kukosa umakini.