Home CAF AL AHLY WAENDELEZA UBABE AFRIKA…WATINGA NUSU FAINALI KLABU BINGWA KWA KISHINDO…

AL AHLY WAENDELEZA UBABE AFRIKA…WATINGA NUSU FAINALI KLABU BINGWA KWA KISHINDO…


Al Ahly wamefanikiwa kuendelea na kampeni ya kutetea taji lao la Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Raja Casablanca kwenye dimba la Stade Mohamed nchini Morocco.

Kikosi cha Pitso Mosimane kikiongozwa na Taher Mohamed, Percy Tau na Hamdi Fathi huku mfungaji bora wa msimu uliopita Mohamed Sherif akianzia benchi kimetinga hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kufuatia matokeo ya jumla (Aggregate) 3-2.

Raja Casablanca ambao waliutawala mchezo huo, waliingia huku wakiwa nyuma kwa mabao 2-1 matokeo waliyoyapata kwenye mchezo wa awali baina ya timu hizo uliopigwa jijini Cairo.

Hata hivyo wamorocco hao walipambana na kufanikiwa kupata bao la mapema lililofungwa na Fabrice Ngoma kwa kichwa katika dakika ya 5 ya mchezo.

Baada ya bao hilo, Al Ahly waliamka na kufanikiwa kupata mkwaju wa penati baada ya mwamuzi kujiridhisha kupitia (VAR), lakini penati hiyo iliyopigwa na Ali Maaloul iliokolewa na kipa wa Casablanca Anas Zniti.

Dakika ya 44, Ahly walifuta makosa yao na kuandika bao la kusawazisha kupitia kwa mlinzi wake Mohamed Abdel Moneim kwa kichwa kufuatia kona iliyopigwa kutoka upande wa kulia na Maaloul na kufanya matokeo kuwa 1-1.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku Al Ahly wakipoteza nafasi katika dakika ya 53 wakati mshambuliaji wake hatari wa kimataifa wa Bafana Bafana,Percy Tau ambaye alikuwa na wakati mgumu kwenye mchezo huo alipokosa bao akiwa yeye na kipa.

Pamoja na kubanwa mbavu kwa sare hiyo, lakini haikuwazuia mafarao hao kutinga hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa kufuatia matokeo ya jumla (Aggregate) ya 3-2 licha ya wenyeji kutawala mchezo kwa kupiga pasi nyingi na kona 11 dhidi ya 2 za wapinzani wao.

SOMA NA HII  BALEKE:- HOROYA WAULIZENI, MTIBWA SUGAR...."NITAHAKIKISHA NAPAMBANA...KWA MKAPA PATACHIMBIKA