Home Habari za michezo EXCLUSIVE…GYAN AFUNGUKA ALIVYOLAZIMISHWA KUFANYA ASIYOYAPENDA NA KIBOSILE WA SIMBA…

EXCLUSIVE…GYAN AFUNGUKA ALIVYOLAZIMISHWA KUFANYA ASIYOYAPENDA NA KIBOSILE WA SIMBA…


UKITAJA majina ya washambuliaji wanaofanya vizuri kwenye Ligi ya Championship huwezi kuacha kulitaja lile la Nicolas Gyan wa DTB aliyefunga mabao 12 akishika nafasi ya pili, huku nafasi ya kwanza akiwa nayo Amissi Tambwe mwenye mabao 14 akichezea timu hiyohiyo.

Mwaka 2017, Gyan alisajiliwa na Simba kama mshambuliaji wa kati akitoka kuifungia timu yake ya Ghana, Dwarfs mabao 11 katika mechi 25, lakini alipotua nchini alijikuta akicheza beki wa kulia nafasi iliyompa changamoto kubwa kuwania namba na Shomary Kapombe.

Katika mahojiano maalumu na Mwanaspoti, Gyan kafafanua zaidi juu ya nafasi hiyo aliyobadilishwa na namna anavyopambana ndani ya DTB. Anasema kubadilishwa namba kumemvurugia madili kwa sababu watu wengi walikuwa wanajua ni mshambuliaji na si vinginevyo.

“Nilipoonekana nacheza beki kwenye CAF kulikuwa na maswali mengi, lakini hakukuwa na namna zaidi ya hivyo, lakini kuna muda nilitaka kugoma ila (kuna) bosi aliniambia niondoke kama sitaki kucheza nafasi hiyo,” anasema.

“Kocha aliniambia nicheze kwa ajili yake na nikafanya hivyo. Unajua hata nilipokuwa Ghana kuna muda nilikuwa nacheza kama winga, lakini sio beki. Maisha ya kucheza kama beki nisiwe muongo yalikuwa magumu kwangu. Sikuwa na furaha lakini ilibidi nicheze kwa sababu hauwezi kugoma.”

APOTEZA NAMBA TAIFA

Gyan anasema kitendo cha kubadilishwa namba kimechangia kwa kiasi kikubwa kukosa nafasi ya kuitwa timu ya Taifa ya Ghana.

“Nimecheza timu zote za vijana kwa kila ngazi na nilikuwa naitwa kama mshambuliaji. Nilikuwa nimebakiza hatua moja tu ya kuitwa timu ya wakubwa, lakini hapohapo ndipo nilibadilishwa namba,” anasema Gyan.

“Nilipokuwa naenda timu za vijana kila mechi nilikuwa nafunga. Yule kiongozi ambaye alinibadili namba kilazima pale Simba sitamsahau, kocha Patrick Aussems aliniomba sana nicheze kwa sababu Kapombe alikuwa ameumia.”

HATAISAHAU AL AHLY

Supastaa huyo anasema upande wa mechi za Ligi Kuu Bara hakukutana na changamoto yoyote, lakini kimataifa ilikuwa balaa na hataisahau mechi dhidi ya Al Ahly kwani alikutana na wachezaji wenye kasi waliompa tabu.

“Kwa sababu haikuwa namba yangu rasmi nilikutana na changamoto nyingi eneo lile, lakini baada ya mchezo huo huku kwenye ligi ilikuwa ni kawaida tu,” anasema.

SIMBA YAMPOTEZEA

Mchezaji huyo anasema baada ya kumaliza mkataba na Simba aliondoka nchini na kurejea kwao Ghana na baadaye alipata dili lingine Uarabuni, ingawa alikumbana na changamoto akiwa nchini Oman.

“Nilipokwenda kule walinipa pesa ya kawaida sana, niliona hakuna sababu ya kusaini, niliamua kurudi nyumbani huku nikiendelea kutafuta madili mengine,” anasema Gyan ambaye alishauriana na staa mwingine wa zamani wa Simba, James Kotei kwenye kucheza nchini humo ingawa, Kotei alicheza timu ya Daraja la Kwanza.

SOMA NA HII  HAJI MANARA AUMBUKA...NI BAADA YA KUMGOMBANISHA RAISI YANGA NA MTANGAZAJI

Gyan anasema baada ya hapo alitimkia Baroka FC ya Afrika Kusini, lakini baada ya kuibuka Uviko-19 wageni wote walitakiwa kurejea nchini kwao.

“Ilikuwa 2021 ile nimeenda Baroka kusaini ndio ukatokea huo ugonjwa, basi tukarudishwa wageni wote na dili la kujiunga nao likafa, nikarejea nyumbani na kujiunga timu ya Legon City,” anasema Gyan.

“Nilicheza nusu msimu tu ligi ya Ghana kwa sababu hakuna pesa sana. Kocha ambaye alinisajili aliondoka na kuja kocha mwingine na wachezaji wake, hivyo sikupata nafasi ya kucheza, niliandika barua ya kuomba kuondoka.”

SIMU YA KIGOGO DTB

Baada ya kuvunja mkataba na Legon City, anasema alipokea simu ya kigogo mmoja wa DTB aliyemtaka ajiunge na timu hiyo na atacheza safu ya ushambuliaji.

“Sikuwa naijua kabisa hii ligi, lakini mimi mwenyewe nilisema mchezaji ni kucheza timu ya daraja lolote, kikubwa unachotakiwa kufanya ni kuwa bora,” anasema Gyan.

“Sikujali kabisa hata nilipojua ipo Championship, bali nilisema nataka niweke rekodi yangu nyingine ya kuipandisha timu Ligi Kuu.”

Anasema akiwa na DTB, kocha Ramadhan Nswazurimo alianza kumchezesha kama winga wa kulia, lakini baadaye aliamua kumfanya kuwa mshambuliaji wa pili.

“Nilianza kucheza kama winga, lakini sasa nacheza eneo langu. Napambana sana nifunge mabao mengi ya kuisaidia timu yangu. Kuhusu kiatu cha ufungaji bora kama nimeandikiwa nitapata, lakini kama sijaandikiwa basi sitapata kwa sababu Mungu ndiye ameandika.”

CHAMPIONSHIP USIPIME

Mshambuliaji huyo anasema Championship ni ngumu na timu ikijisahau kidogo tu basi nyingine zinapita kwa sababu ya ushindani uliopo na pia wachezaji hukamiana kwani wanatumia nguvu zaidi.

“Huku ligi ni nzuri na nafurahia maisha, lakini kuna changamoto ndogondogo kama kukamiwa, japokuwa muda mwingine ni viwanja lakini nimevizoea,” anasema.

Kuhusu mkataba wake anasema: “Naheshimu mtu ambaye amenileta hapa, kwa hiyo lazima niwape kipaumbele. Wakishindwa kunibakisha basi nitaondoka, lakini kama wakinipa kile nitakachohitaji nitabaki hata kama tupo Ligi Kuu. Wapo watu ambao wameanza kuchati na mimi, lakini sijui wametoka wapi, lakini najua ni viongozi wa timu kutokana na maswali ambayo wanayoniuliza.”

JEZI YA NJANO

Gyan anasema anashangazwa na mashabiki aliodai huenda ni wa Simba kumshangaa kila anapovaa jezi ya DTB ambayo ni njano.

“Mchezaji huwa anahama mara kwa mara. Kama unampenda mchezaji basi unatakiwa umpende yeye tu na sio kitu kingine. Akienda popote inabidi uwe naye, nashangaa nikivaa jezi ya timu yangu mashabiki hunishangaa,” anasema Gyan.

“Kila mchezaji ana familia, kwa hiyo ofa inapokuwa nzuri lazima atoke na kwenda kucheza katika timu ambayo itampa mshahara mzuri ili aendeshe familia na ukiona mchezaji amebaki kwenye timu moja, basi anapewa kile alichoridhika nacho.”