Home Habari za michezo KUELEKEEA MSIMU UJAO NA LIGI YA MABINGWA…..’TEKERO’ AWAPA YANGA MASHINE TATU ZA...

KUELEKEEA MSIMU UJAO NA LIGI YA MABINGWA…..’TEKERO’ AWAPA YANGA MASHINE TATU ZA KAZI…


Nyota wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Abeid Mziba ‘Tekero’ amekiangalia kikosi cha sasa cha Yanga kinachoongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara na kuwaambia mabosi wa klabu hiyo, “ongezeni watu wa maana ili mmalize kazi.”

Mziba alisemakuwa, mabosi wa Yanga wanatakiwa kuongeza mabeki wawili wa kazi ili kusaidiana na waliopo kujiweka mguu sawa kwa ajili ya mechi za kimataifa msimu ujao.

Pia alisema mbali na kuongeza mabeki wawili, lakini mabosi wa Yanga wanatakiwa kusajili watu wa maana katika maeneo mengine ili kuwasaidia mastaa waliopo sasa kikosini hasa eneo la ushambuliaji ili kufanya vyema kwenye mechi hizo za kimataifa kwa msimu ujao.

“Yanga ya sasa inahitaji beki wa kushoto mwenye uwezo wa kukaba, beki wa kati wa kusaidiana na Dickson Job na Bakari Mwamnyeto sio kwamba waliopo ni wabaya, ila ni lazima kuwe na mbadala kwani anaweza mmoja wao au wote kuumia,” alisema.

Mziba aliyeitumika Yanga kwa miaka 12 kuanzia 1980-1992 alisema licha ya Yanga kufanya vizuri katika ligi ya ndani, pia inatakiwa kufanya usajili wa nyota wenye uwezo na uzoefu wa michuano ya kimataifa kuepuka aibu ya kutolewa mapema.

“Pale mbele kwa Fiston Mayele lazima awe na msaidizi wake angalia akitoka au akiumia pale hakuna kitu lazima tuwe na mshambuliaji wa kulazimishia, mpira ni sayansi lazima uwekeze ndani ya uwanja kwa kutafuta wachezaji sahihi ambao watakupa matokeo mazuri,” alisema mkali huyo wa zamani wa mabao ya vichwa.

“Sehemu ambayo tupo vizuri na wala hatuhitaji kufanya mabadiliko ni pale katikati wale waliopo ni wachezaji sahihi hatuhitaji kuongeza mtu yeyote,” aliongeza Mziba.

Aidha mkali huyo aliyewahi kuzichezea pia timu za Ufundi Kigoma, Reli Morogoro na Reli Dodoma kabla ya kutua Yanga mwaka 1980, alisema anasikitishwa na kuwepo kwa idadi ndogo ya mabao ya vichwa yanayofungwa katika ligi mbalimbali nchini na kushauri wachezaji kuzitumia nafasi wanazozipata.

Mziba aliweka mapenzi yake kando na kuifagilia Simba kwa kufika robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa kusema; “Wapo vizuri nje na ndani ya uwanja na kubwa wanaliwakilisha vizuri Taifa, kwa hili nawapongeza.”

SOMA NA HII  AHMED ALLY: VIPERS WATAJUTA KUJA KUCHEZA NA SIMBA DAR.....MOTO UTAWAHUSU...

Msimu huu Yanga ilishiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini ikatolewa raundi ya awali kwa kufungwa nje ndani na Rivers United ya Nigeria, huku Simba iking’oka raundi ya kwanza kwenye michuano hiyo dhidi ya Jwaneg Galaxy ya Botswana na kuangukia Kombe la Shirikisho iliyopo hadi sasa ikiwa robo fainali.

KIUNGO FUNDI

Wakati Mziba akitoa mapendekezo hayo, inaelezwa tayari mabosi wa Yanga wameanza msako wa nyota wapya kwa msimu ujao, ikianza kumnyemelea kiungo fundi wa Mbeya City, Aziz Andambwile na mshambuliaji George Mpole wa geita Gold.

Habari za ndani kutoka kwa watu wa karibu wa wachezaji hao zimethibitisha kuwa, Yanga imewasiliana nao, lakini wametakiwa kumalizana na viongozi wa klabu wanazozichezea kwa sasa mabao hata hivyo jana walitafutwa bila mafanikio licha ya simu zao kuwa hewani.

Andambwile aliyesajiliwa na Mbeya City kutoka Big Bullets ya Malawi na Mpole wameonyesha soka tamu wakiwa na timu zao kiasi cha kumfanya kocha wa Taifa Stars, Kim Paulsen alimuita katika timu iliyocheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Afrika ya Kati na Sudan zilizochezwa mwishoni mwa mwezi uliopita.