Home Habari za michezo KUELEKEA MECHI DHIDI YA NAMUNGO LEO….SIMBA WAANIKA HAYA KUHUSU KESI YA MORRISON…

KUELEKEA MECHI DHIDI YA NAMUNGO LEO….SIMBA WAANIKA HAYA KUHUSU KESI YA MORRISON…


MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba, baada ya kutoka suluhu dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga, leo watakuwa kwenye Uwanja wa Ilulu mjini Lindi kucheza dhidi ya Namungo.

Utakuwa ni mchezo wa 21 kwa upande wa Simba, huku Namungo ikicheza mechi 22, zikifuatana kwenye msimamo, mabingwa watetezi wakiwa na pointi 42, wenyeji wa mechi hiyo wakiwa na alama 29.

Wakati Simba ikijaribu kuufukuzia ubingwa ambao unaonekana kabisa kuelekea kwa watani wa wa jadi, Yanga, Namungo itakuwa ikizitafuta pointi tatu kwa ajili ya kung’ang’ania kwenye nafasi ya tatu ili kupata tiketi ya kucheza mechi za kimataifa msimu ujao.

Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema kati ya wachezaji waliosafiri, yupo Bernard Morrison ambaye alishikiliwa na Jeshi la Polisi kwa saa chache Jumamosi baada ya mechi kati ya Yanga dhidi ya Simba kwa madai ya kumjeruhi shabiki.

“Tunakwenda kucheza mechi nyingine leo, pamoja na kwamba ratiba imebana sana. Jumamosi tumecheza na Yanga, siku hiyo hiyo tukawapa ruhusa wachezaji wetu, kesho yake Jumapili wakarejea mazoezini, leo tupo kwenye mechi. Kiukweli imebana sana hata kocha wetu Pablo (Franco), amelalamikia hili, lakini hakuna namna ni lazima tupambane,” alisema.

Alisema siku zote mechi dhidi yao na Namungo inakuwa na mvuto na ushindani mkubwa kutokana na wapinzani wao kuwa na wachezaji wazoefu kwenye ligi, baadhi wakiwa wamepita kwenye kikosi hicho.

Kuhusu sakata la Morrison amesema kuwa hawezi kusema lolote zaidi ya kuwaachia Jeshi la Polisi lifanye kazi yake, lakini alithibitisha kushikiliwa kwa saa kadhaa.

“Ni kweli Morrison alishikiliwa kwa saa kadhaa, lakini akaachiwa na akajiunga na wenzake kambini, na amesafiri na wenzake, yupo fiti kwa ajili ya mechi ya Namungu, suala hilo tumeliacha kwa Jeshi la Polisi, yaliyotokea si ndwele tugange yajayo, maisha yanaendelea kama kawaida,” alisema Ahmed.

Hata hivyo, kwenye mechi hiyo, Simba itamkosa Saido Kanoute ambaye aliumia kwenye mechi dhidi ya Yanga ambaye alibaki Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu.

SOMA NA HII  THOMAS ULIMWENGU ACHEKELEA KURUDI TANZANIA

“Tumekuja na wachezaji wote, kasoro Kanoute ambaye aliumia kwenye mechi ya Yanga, amebaki ili kupata vipimo ili kuangalia kwa kiasi gani aliumia, ili aanze matibabu. Baada ya kufanyika vipimo tutawaeleza.”

Wakati huo huo, beki kisiki wa timu hiyo, Henoc Inonga ‘Varane’, amekunwa na namna mashabiki wa timu hiyo wanavyoonyesha mapenzi makubwa kwa timu yao kila wanapokwenda.

Inonga alitoa kauli hiyo baada ya kikosi cha Simba kuwasili Mtwara jana asubuhi na kupata mapokezi makubwa huku jina lake likiimbwa na mamia ya mashabiki waliojitokeza kuwalaki kutokana na kazi kubwa aliyoifanya ya kumdhibiti mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele, kwenye mechi ya ‘dabi’ Jumamosi iliyopita ambayo ilimalizika kwa sare tasa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.

‘Mashabiki wetu wanaonyesha mapenzi makubwa kwetu, hii inatuongezea morali hata tukiwa uwanjani kujituma kuhakikisha tunawapa furaha. Bado hatujakata tamaa ya ubingwa, tutaendelea kupambana hadi mechi yetu ya mwisho, tunajua haitakuwa rahisi, lakini hakuna kinachoshindikana,” alisema.

Naye Meneja wa Namungo, Steven Josiah, amesema kuwa kwa sasa kikosi chao kipo kwenye mazoezi makali kujiandaa na mechi hiyo, huku akitaraji kupata ushindi kwenye mechi hiyo wakitaka kulipiza kisasi baada ya kufungwa bao 1-0 kwenye mechi ya mzunguko kwa kwanza lililofungwa dakika za majeruhi na Meddie Kagere.

“Nguvu kubwa tunayoiweka kwa sasa ni kuhakikisha tunapata matokeo mazuri kwenye mechi zote zinazokuja, ikiwamo hii ya Simba, lengo letu turejee tena kwenye michuano ya kimataifa, alisema meneja huyo.