Home Habari za Yanga SENZO :- SIMBA WANATAKIWA KUSHUKURU KUPATA SARE NA YANGA…LA SIVYO HALI INGEKUWA...

SENZO :- SIMBA WANATAKIWA KUSHUKURU KUPATA SARE NA YANGA…LA SIVYO HALI INGEKUWA MBAYA KWAO…


YANGA imetoa tamko kwamba bado inajiuliza imewakosaje watani wao Simba katika pambano lao la Kariakoo Dabi juzi Jumamosi, licha ya kukiri pointi moja waliyoipata inakwenda kuongeza kitu wakihesabu siku za ubingwa, kisha hapo hapo ikawaambia Simba “shindeni dhidi ya Pamba tuje tufunge rasmi msimu.”

Simba na Yanga zilivaana juzi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na kutoka suluhu ikiwa ni mara ya pili katika Ligi Kuu Bara msimu huu, huku timu hizo zikiendelea kutofautiana pointi 13 katika msimamo, Yanga ikiwa kileleni na alama 55 dhidi ya 42 za watani wao.

Timu hizo zimesaliwa na mechi pekee ya michuano ya Kombe la Shirikisho (ASFC) hatua ya nusu fainali ambayo Yanga imeshatangulia mapema kwa kuing’oa Geita Gold katika robo fainali na Simba inasubiri Mei 14 kujua hatua yake dhidi ya Pamba baada ya awali pambano lao la hatua hiyo kuahirishwa Aprili 13.

Mtendaji Mkuu wa Yanga, Senzo Mazingisa, alisema mchezo wa watani kuisha kwa suluhu hayakuwa matokeo ya kwanza waliyoyatarajia lakini bado wanataka ushindi dhidi ya Simba.

Senzo alisema wanaiombea Simba iifunge Pamba kisha wakutane tena kwenye mchezo wa nusu fainali ya ASFC ili waweze kufunga msimu katika mchezo huo ambao lazima mshindi apatikane.

“Tulidhani ushindi ungekuwa kwetu leo (juzi) lakini haikuwa hivyo ingawa hii pointi moja sio kitu kibaya kwetu kwa kuwa hesabu zetu za kwanza ni ubingwa, hii inakwenda kuongeza kitu kwetu,” alisema Senzo ambaye amewahi kuwa Mtendaji Mkuu Simba kabla ya kutimkia Yanga.

“Yanga bado inatamani kushinda mbele ya Simba, hii ni mechi ya pili kwenye ligi tunatoka sare, ingawa tulishawafunga katika ufunguzi wa ligi, tunaweza kukutana nao katika hatua ya nusu fainali nafikiri tuwaombee washinde ili tukutane tufunge msimu.

Yanga tayari ilishatinga hatua ya nusu fainali baada ya kuwafunga Geita Gold kwa bao 1-0 huku Simba wakisubiri kukutana na Pamba baada ya awali mchezo huo kusogezwa mbele.

Senzo aliongeza kuwa matokeo ya sare dhidi ya Simba, wekundu hao wanatakiwa kuyapokea kwa mikono miwili ambapo wangepoteza inawezekana moto mkubwa ungewaka ndani ya klabu hiyo.

SOMA NA HII  HIVI NDIVYO DUBE ANAVYOZIGONGANISHA SIMBA NA YANGA...ISHU YAKE YAPAMBA MOTO...

Alisema anaijua Simba hali isingeweza kupita kirahisi kama wangepoteza mchezo huo wakifuatia kutolewa kwenye Kombe la Shirikisho huku pia Yanga wakichukua taji la ligi.

“Haya matokeo nadhani yanatakiwa kupokelewa kwa mikono miwili kwa wapinzani wetu.”