Home Habari za michezo KISA ‘MAVITUZI’ YA SAKHO….WASUDANI WAIWEKEA SIMBA MEZANI BILIONI 1.3…VIONGOZI WAJING’ATA NG’ATA…

KISA ‘MAVITUZI’ YA SAKHO….WASUDANI WAIWEKEA SIMBA MEZANI BILIONI 1.3…VIONGOZI WAJING’ATA NG’ATA…


WINGA kutoka Senegal, Pape Ousmane Sakho, amewagawa mabosi wa Simba baada ya Waarabu kutoka Sudan kutoa ofa ya donge nono ili kumng’oa Msimbazi.

Mabosi wa Simba wamepokea ofa ya Dola 600,000 (Sh1.3 bilioni) kutoka klabu ya Al Hilal ya Sudan ikimhitaji Sakho, lakini historia ya kilichotokea baada ya kuuzwa kwa Luis Miquissone na Clatous Chama mwishoni mwa msimu uliopita imewafanya wagawanyike katika kutoa uamuzi wa kuruhusu au kutomruhusu nyota huyo aondoke.

Habari za uhakika ambazo zinasema kuwa baadhi ya viongozi wa Simba wapo tayari kumuachia nyota huyo mwenye umri wa miaka 25 waliyemsajili msimu huu kutoka Teungueth FC ili kupata fungu hilo nono la Wasudani wakiamini zitatosha kuwapatia wachezaji wengine mahiri watakaoziba pengo lake.

Hata hivyo, vigogo wengine wa Simba, wanaonyesha kutokuwa tayari kumruhusu Sakho aondoke kwa hofu ya kuvuruga kikosi chao na kukosa mbadala wake kama ilivyotokea mwaka jana walipowauza Luis kwa Al Ahly ya Misri na Chama kwa RS Berkane ya Morocco, japo Mzambia huyo alirejea katika dirisha dogo na sasa ana mabao matatu ya Ligi Kuu.

“Kuna ofa ya kiasi cha Dola 600,000 imekuja kutoka kwa timu moja ya nje ikimhitaji Sakho, lakini klabu inasitasita kumuuza kwa kuogopa kisije kutokea kama kile cha mwanzoni mwa msimu huu baada ya kina Chama kuondoka,” kilisema chanzo toka ndani ya Simba.

“Lakini wapo wanaotaka aruhusiwe kuondoka kwa vile nafasi anayocheza ya wingi ina wachezaji wenye kuimudu vyema, pia upo uwezekano wa kutumia fedha za mauzo yake kusajili wachezaji wapya kwa sababu kuna mawinga wengi Afrika tena klabu isingetumia gharama kubwa.”

Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alikiri ni kweli klabu hiyo imepokea ofa hiyo ila haikuwa kwa ajili ya dirisha lijalo la usajili.

“Ofa iliyokuja klabuni ilitoka Al Hilal kwa kiasi hicho cha Dola 600,000 ikimhitaji Sakho lakini wao walitaka uhamisho huo ufanyike Aprili mwaka huu kwa vile ndio ulikuwa muda wa dirisha la usajili huko kwao,” alisema Ahmed.

SOMA NA HII  PAMOJA NA KUFUNGIWA VIOO KUCHEZA YANGA...KOCHA KASEMA NI MUKOKO NA MAYELE TU..AFUNGUKA KILA KITU...

“Hatukuwa tayari kumuachia kwa kipindi hiki kwani ligi bado inaendelea na dirisha kwa hapa kwetu litakuwa limefungwa tusingeweza kupata mbadala wake, ila tuliwaambia tupo tayari kuwauzia ligi ikimalizika, jambo ambalo hatukufikia muafaka. Lakini kama wakija tena baada ya ligi kumalizika, milango ipo wazi na sio wao tu bali timu yoyote ambayo itakuwa tayari kuweka kiasi kile ambacho tunakihitaji.”

Sakho ni miongoni mwa nyota wanaofanya vyema katika kikosi cha Simba msimu huu, hasa katika mashindano ya kimataifa ambayo Simba imetolewa katika hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Katika mashindano hayo, nyota huyo amefunga mabao mawili dhidi ya Asec Mimosas na RS Berkane ambayo yote yalichaguliwa kuwa mabao bora ya wiki.

Sakho mwnye bao moja katika Ligi Kuu, alijiunga na Simba, Julai mwaka jana akitokea Teungueth ya Senegal ambako alikuwa mchezaji bora wa msimu uliopita.