Home Habari za michezo MATAJIRI WA LIGI DARAJA LA KWANZA DTB KUUNGANA NA SIMBA NA YANGA...

MATAJIRI WA LIGI DARAJA LA KWANZA DTB KUUNGANA NA SIMBA NA YANGA LIGI KUU MSIMU UJAO…


TIMU ya DTB imefanikiwa kupanda Ligi Kuu Bara msimu ujao baada ya jana kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Pamba, mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi.

Bao la timu hiyo lilifungwa na Joel Madondo dakika ya 75, aliyeingia kipindi cha pili akichukua nafasi ya Tafadzwa Kutinyu ambaye hakuwa na mchezo mzuri.

Kipindi cha kwanza kilianza kwa timu zote kushambuliana licha ya wenyeji DTB kutawala zaidi mchezo kutokana na ubora wa nyota wengi kwenye kikosi hicho.

Pamba inayonolewa na kocha, Wilbert Mweta ilicheza kwa nidhamu ya hali ya juu sana kwa kuwaheshimu wapinzani wao na hadi dakika 45, za kipindi cha kwanza zinamalizika timu hizo zilitoka suluhu ya bila ya nyavu kutikiswa.

Kipindi cha pili, DTB inayofundishwa na Kocha Mrundi, Ramadhan Nswanzirimo ilishambulia lango la Pamba kwa kasi huku washambuliaji wake wakikosa umakini wa kumalizia nafasi za kufunga.

Licha ya kosakosa nyingi kwa DTB ila shujaa wa kikosi hicho alikuwa ni Joel Madondo aliyeipatia bao muhimu timu hiyo dakika 75, na kuipatia tiketi ya moja kwa moja kucheza Ligi Kuu Bara msimu ujao.

Timu hiyo ilikuwa ikihitaji ushindi wa aina yeyote kujihakikishia kucheza Ligi Kuu Bara kutokana na kufikisha pointi 65 ambazo hakuna timu yeyote inayoshika kuanzia nafasi ya tatu hadi ya 16, itazifikia.

Huu ni mchezo wa pili msimu huu kwa Pamba kupoteza dhidi ya DTB kwani mzunguko wa kwanza uliopigwa Januari Mosi, 2022, katika Uwanja wa CCM Kirumba ilifungwa pia bao 1-0.

Kwa sasa DTB itakamilisha ratiba tu katika michezo miwili ijayo ugenini ikianza na Mashujaa ya Kigoma Mei 14, kisha kuhitimisha msimu kwa kumenyana na Kitayosce ya Tabora Mei 21.

DTB inashika nafasi ya kwanza na pointi 65 baada ya kucheza michezo 28, ikishinda 20, sare tano na kufungwa mitatu, huku Pamba inasalia nafasi ya tisa na pointi 36, baada pia ya kucheza michezo 28.

SOMA NA HII  IMEFICHUKAA...HII HAPA SABABU YA AZIZ KI KUTOKURUDI NA TIMU YANGA...CHANZO NI...