Timu ya Taifa ya Tanzania kwa mpira wa mguu kwa walemavu Tembo Warriors, imepata mwaliko rasmi wa kushiriki mashindano ya Ulaya itakayofanyika nchini Poland.
Mashindano hayo yanayojulikana kama Amp-Futbal Europe 2022 yanatarajia kufanyika mwezi Juni kati ya tarehe 10 hadi 13 katika mji wa Warsaw nchini Poland.
Mashindano haya yanatarajia kushirikisha nchi nne, nchi tatu kutoka bara la ulaya ambazo ni England, Italy na Poland, na nchi moja kutoka Africa. Na hivyo Tanzania ndiyo nchi pekee ya africa iliyopata mwaliko kati ya nchi 18 za Africa na nchi ya pekee kati ya nchi nne za Africa zilizofuzu kwenda kombe la Dunia.
Rais wa Shirikisho la mpira wa miguu kwa walemavu Tanzania TAFF ndg. Peter Sarungi amesema kwamba, Tanzania inazidi kung’ara katika mchezo huu na hii inatokana na ushiriki wa Serikali yetu na wadau wengine kusaidia kulea na kuhudumia mchezo huu nchini.
Mfano mzuri uliochukuliwa na mataifa mbalimbali ya nje ni utayari na ukubali wa Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali yake kugharamia na kuandaa mashindano ya Africa (CANAF 2021) ambayo yamesaidia Africa kupata wawakilishi wa kwenda kombe la Dunia.
Pia Sarungi amesema kuwa Tembo Warriors imekuwa ni timu yenye vijana wengi kuliko timu nyingi za Ulaya na wameonekena wanafanya vizuri hasa kwa wale walioshiriki mashindano ya Africa na wale ambao wamepata nafasi ya kwenda kucheza mpira wa kulipwa.