Chama cha Soka Ulaya (Uefa) kimetangaza mfumo mpya wa mashindano yake yote matatu, huku kikisema kuwa mradi wa kuanzisha Super League sasa umezikwa “kwa angalau miaka 20”.
Baada ya kikao cha mkutano mkuu uliofanyika jijini Vienna, Australia, rais wa Uefa, Aleksander Ceferin alisema baada ya mashauriano ya muda mrefu hatimaye wamefikia uamuzi wa kupanua mashindano hayo matatu kwa kuongeza timu nne na kuondoa hatua ya makundi na kwamba mfumo huo utaanza msimu wa mwaka 2024/25.
Uamuzi huo wa mkutano mkuu ni mwendelezo wa uamuzi uliofanyika Aprili 19 wa kuanzisha mfumo unaoitwa “Swiss system”.
Mabadiliko makubwa katika mfumo huo ni kupunguza idadi ya mechi kutoka 10 hadi nane katika hatua ya ligi ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya na kubadili vigezo vya kutoa nafasi mbili kati ya nne za nyongeza za kucheza ligi hiyo kubwa.
Katika hilo, Uefa imeondoa pendekezo la awali la kutoa nafasi mbili kwa klabu zenye historia ya kufanya vizuri katika mashindano hayo hata kama zitakuwa hazijafuzu kushiriki Ligi ya Mabingwa kutoka katika nchi zao.
“Hii inaonyesha jinsi Uefa inavyoheshimu kanuni za ushindani wa wazi na kupata nafasi kutokana na kufuzu, huku ikitambua haja ya kulinda mashindano ya ndani katika nchi wanachama,” imeandika tovuti ya Uefa.
Mechi nane za Ligi ya Mabingwa zitachezwa ndani ya Wiki Kumi za Ulaya kwa mujibu wa uamuzi wa Aprili, 2021. Ligi ya Mabingwa wa Ulaya, Ligi ya Europa na Ligi ya Conference zitakuwa na wiki peke katika kalenda ya Uefa.
Nafasi nne zilizopatikana kutokana na kuongeza timu kutoka 32 hadi 36 katika hatua ya ligi ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya zimewekewa vigezo.
Nafasi moja, kw amujibu wa uefa.com, itakwenda kwa timu itakayoshika nafasi ya tatu ya mashindano ya nchi ambayo inashika nafasi ya tano katika orodha ya ubora ya nchi wanachama wa Uefa.
Nafasi moja itapewa bingwa wa nchi wanachama kw akuongeza idadi kutoka timu nne hadi tano katika idadi ya klabu zinazofuzu kwa kupitia njia inayoitwa “Champions Path”.
Nafasi mbili za mwisho zitakwenda kwa nchi wanachama ambazo klabu zake zilifanya vizuri katika msimu uliotangulia (jumla ya idadi ya pointi zilizopatikana kwa kugawanya na klabu shiriki). Nchi hizo mbili zitapata nafasi moja kwa klabu iliyoshika nafasi bora chini ya zile za nchi za kushiriki Ligi ya Mabingwa.
Kwa mfano, Uefa.com imeripoti, mwishoni mwa msimu huu nchi hizo mbili ambazo zingepata nafasi hizo kwa kutegemea matokeo ya jumla ya kufanya vizuri kwa klabu zake, zingekuwa Uholanzi na England.
Uefa pia imesema kuwa mechi zote za michuano yake zitachezwa katikati ya wiki, ikitambua umuhimu wa mashindano ya ndani ya nchi wanachama barani Ulaya.
“Uamuzi wa leo umehitimisha mazungumzo marefu ya mchakato wa mashauriano ambayo tulihusisha mawazo ya mashabiki, wachezaji, walimus, vyama vya kitaifa, klabu na ligi kw auchache, lengo likiwa ni kupata suluhisho bora kwa ajili ya maendeleo na mafanikio ya soka barani Ulaya, katika hatua zote za ndani ya nchi na kimataifa,” alisema rais huyo wa Uefa.
Kwa kuongeza idadi kutoka 32 hadi 36 katika Ligi ya Mabingwa wa Ulaya, badiliko la msingi litakuwa kuachana na hatua ya makundi na kuwa na ligi moja inayojumuisha timu zote shiriki.
Kila timu sasa itakuwa na uhakika wa kucheza mechi nane dhidi ya wapinzani nane tofauti (mechi nne nyumbani na nne ugenini) badala ya mechi sita dhidi ya timu tatu zilizokuwa zikichezwa nyumbani na ugenini.
Timu zitakazoshika nafasi nane za juu zitafuzu kucheza hatua ya mtoano, wakati timu zitakazoshika nafasi ya tisa hadi 24 zitakutana katika mechi za mtoano za nyumbani na ugenini ili kukata tiketi ya kucheza hatua ya 16 bora.
Muundo wa aina hiyo pia utatumika katika mashindano mengine mawili ya Uefa (mechi nane katika Ligi ya Europa) na mechi sita katika Conference, mashindano yote hayo yakiwa na timu 36.
Katika uamuzi mwingine, Uefa imesema mpango wa kuanzisha Super League umezikwa rasmi na kama utaibuka basi ni baada ya miaka 20.
“Sitaki kuiita Super league kwa sababu ni kila kitu na si Super League,” alisema Caferin ambaye ni raia wa Slovenia.
Klabu 12 kati ya klabu kubwa barani Ulaya zilisaini mpango wa kuanzisha ligi hiyo Aprili mwaka jana, lakini ukafa ndani ya siku chache baada ya kupingwa vikali na wachezaji na mashabiki, hali kadhalika serikali na vyama vya soka.
Klabu tisa zilijitoa na kuziacha Real Madrid, Barcelona na Juventus zikiendelea na mpango huo.
Ceferin alisema klabu hizo tatu hazina uwezo wa kufufua mpango huo.
“Kwangu mpango huu umekufa kabisa au labda kwa miaka 20. Sijui kitakachotokea baadaye,” alisema katika mkutano na waandishi wa habari.
Hakutaka kutaja hatua za kinidhamu zitakazochukuliwa dhidi ya vigogo hao watatu.
Mwezi Aprili, jaji wa Madrid alikubaliana na rufaa ya Uefa na kuondoa kinga ya adhabu kwa klabu hizo iliyotolewa na mahakama nyingine mapema mwaka huu.
Kesi inaendelea katika Mahakama ya Umoja wa Ulaya baada ya mahakama ya Hispania kuhoji kama Uefa inatumia vibaya mamlaka yake.
“Tunaheshimu mahakama na kusubiri uamuzi wa mwisho, hatuna haraka,” alisema Caferin, mwanasheria wa michezo kabla ya kuingia katika uongozi wa soka.