WAKATI kocha Pablo Franco ameendelea kupiga hesabu za kavuna alama zote 21 kwenye mechi saba zilizosalia za Ligi Kuu ili kuongeza presha ya mbio za ubingwa, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez, amefunguka kuhusu usajili wa kibabe kwa ajili ya msimu ujao kwa mechi za ndani na za kimataifa.
Hadi sasa Simba ipo nafasi ya pili kwenye msimamo ikiwa na pointi 49 nyuma ya vinara Yanga wenye alama 57 wakiongoza kwa tofauti ya alama nane zikiwa na michezo sawa (23) na sasa Pablo amepanga kushinda mechi zote saba zilizobaki ili kufikisha pointi 70, huku akiiombea Yanga ipoteze tatu au mbili na sare mbili, ili waweze kutetea ubingwa.
Ili kuhakikisha hilo linatokea, Pablo ameeleza kuwapa nafasi wachezaji wake wote waliofiti ili kuepuka uchovu kwa baadhi yao kutokana na ratiba kuwa na muda mfinyu wa mapumziko.
“Kwenye mechi iliyopita (dhidi ya Kagera) tuliwakosa wachezaji wetu wengi walio majeruhi lakini hatuwezi kulalamika inabidi tuendelee kupambana na kuwatumia hawa waliopo.
“Hauwezi kucheza na wachezaji wale wale kila baada ya siku tatu, unahitaji kutoa muda wa maandalizi na mapumziko kwa wengine,” alisema Pablo na kuongeza;
“Bado tupo kwenye mbio za ubingwa, tunacheza tofauti kutokana na tathmini tunayoifanya juu ya wapinzani hivyo lazima tubadili wachezaji ambao wataendana vyema na vile tunavyokuwa tunataka kucheza kwani muda wa mapumziko ni mfupi na tunahitaji kushinda kila mechi.”
Mechi zilizobaki za Simba ni dhidi ya Azam, Geita Gold, Tanzania Prisons, Mbeya Kwanza (ugenini) na KMC, Mbeya City na Mtibwa Sugar itakazokuwa nyumbani.
Kwa upande wa Yanga imebakiza mechi na Dodoma Jiji, Biashara United, Mbeya City (ugenini) na Mbeya Kwanza, Coastal Union, Polisi Tanzania na Mtibwa itakazocheza nyumbani.
BARBARA HUYU HAPA
Simba imekuwa ikihusishwa kuwasajili baadhi ya wachezaji kama, Victorien Adebayor na wengineo kwa ajili ya kuboresha kikosi chao msimu ujao na Barbara amesema kuwa kabla ya kishindo cha usajili wa nyota wapya, wataanza kuongeza mikataba ya waliopo kikosini.
Barbara alisema kuna baadhi ya wachezaji wamekuwa kwenye viwango bora na kutoa mchango kwa ajili ya timu kuhakikisha inafanya vizuri ni ngumu kuachana nao mara baada ya mikataba yao kumalizika.
Alisema: “Halitakuwa jambo zuri kwa wachezaji wetu kuona wapya wanasajiliwa wakati wao walio kwenye kuipigania timu kufanya vizuri mikataba yao inamalizika na hawajaongezewa mipya.
“Tutaanza kwanza na kuwaongeza mikataba wachezaji muhimu ambao mwisho wa msimu huu inamalizika na baada ya kumalizana nao hapo tutaangalia mahitaji mapya ya timu kwa kumsikiliza kocha.
“Wakati huu nimetingwa pamoja na kuzidiwa na majukumu mengi kuhakikisha tunakamilisha zoezi hilo la kuwaongeza mikataba mipya wachezaji wetu na baada ya hapo akili itatulia kufanya mengine yafuatayo.”
Kwenye kikosi cha Simba wachezaji wanaomaliza mikataba mwisho wa msimu huu ni Erasto Nyoni, Joash Onyango, Chriss Mugalu, Aishi Manula, Hassan Dilunga, Mzamiru Yassin, Pascal Wawa na Meddie Kagere.
NJIA NYEUPE
Chanzo cha kuaminika kimesema kuwa kuna wachezaji wanaofikia 15 ambao njia ni nyeupe kwao kuondoka kutokana na sababu mbalimbali huku wachezaji wengine wakiingia katika sintofahamu baina ya uongozi na benchi la ufundi kama wabaki ama waondolewe katika ujenzi wa Simba mpya ya hatari.
Wachezaji walioingia kwenye mjadala kutokana na sintofahamu ni pamoja na Sadio Kanoute, Peter Banda na Kibu Denis huku Pape Sakho akiwa kwenye mjadala wa kuuzwa baada kutakiwa na Al Hilal ya Sudan.
Wachezaji ambao njia yao ni nyeupe kuondoka ni Chris Mugalu, Taddeo Lwanga ambaye majeraha yanamponza.