Bao alilofunga Straika George Mpole limemfanya kuongoza katika orodha ya wafungaji Ligi Kuu akimuacha mpinzani wake, nyota wa Yanga Fiston Mayele.
Leo akiiongoza Geita Gold dhidi ya Mbeya Kwanza katika mchezo uliopigwa uwanja wa Majimaji mjini Songea, Mpole alitumia dakika 11 tu kuwaua wapinzani hao na kumuongezea Mayele presha zaidi ambaye amecheza mechi tatu mfululizo bila ‘kutetema’.
Mpole alifunga bao hilo baada ya kutokea piga nikupige langoni mwa wapinzani wao na mpira kumkuta mfungaji huyo eneo sahihi na kukunjua shuti lililomshinda Kipa Hamad Kadedi.
Hata hivyo Mbeya Kwanza walipambana kusawazisha lakini mabeki wa Geita Gold walikuwa imara kudhibiti hatari zote zilizolenga lao lao na kufanya dakika 45 za kwanza kumalizika kwa wenyeji kwenda mapumziko wakiwa nyuma kwa 1-0.
Kipindi cha pili wenyeji ndio walianza kufanya mabadiliko, ambapo Eliuta Mpepo na Issa Kanduru waliwapisha Oscar Mwajanga na Edgar William dakika ya 56 huku Geita wakiwatoa Raymond Masota na kumwingiza Hassan Ramadhan dakika ya 63 na Edmund John kumpisha Juma Mahadhi dakika ya 84
Hata hivyo Mbeya Kwanza walipata pigo kwa kucheza pungufu baada ya Straika wake, Enock Jiah kuoneshwa kadi nyekundu baada ya kadi mbili za njano dakika ya 74 na kuwafanya vibonde wao kumaliza dakika takribani 15 za mwisho wakiwa pungufu.
Kwa matokeo hayo, Mbeya Kwanza wanabaki mkiani kwa pointi 23 na kuendelea kuwa kwenye wakati mgumu wa kukwepa kushuka daraja, huku Geita Gold wakichumpa hadi nafasi ya tatu kwa alama 34.