Mshambuliaji wa Yanga, Chico Ushindi nafasi yake ya kucheza ndani ya kikosi hicho inaonekana kuwa ngumu baada ya kuwa nje ya uwanja mara kwa mara kutokana na majeraha anayopata.
Ushindi alijiunga Yanga kwenye dirisha dogo la usajili la Januari msimu huu akitokea TP Mazembe ya DR Congo lakini hajawa na wakati mzuri kwenye timu hiyo.
Mshambuliaji huyu awali alianza kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Mbuni na baada ya hapo kwenye mechi za Ligi Kuu alikaa benchi mchezo dhidi ya Polisi Tanzania aliingia dakika 78 akichukua nafasi ya Jesus Moloko.
Mchezo mwingine wa Ligi uliofuata dhidi ya Mbeya City staa huyo aliingia dakika 82 huku mchezo ukimalizika kwa 0-0.
Baada ya hapo Ushindi alianza kuumwa nyama za paja na alikosa mechi za tatu dhidi ya Mtibwa Sugar, Kagera Sugar na Geita Gold.
Alirejea tena uwanjani kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya timu ya Taifa Somalia huku akifunga bao kwenye sare 1-1.
Mshambuliaji huyu alianza mchezo dhidi ya KMC ambao alitoa pasi ya bao baada ya kupiga kona iliyoungwa na Djuma Shabani kwa kichwa na mpira kwenda wavuni.
Baada ya mchezo huo Ushindi alikuwepo kwenye benchi katika mechi ya kirafiki dhidi ya Mafunzo na baada ya hapo hajaonekana uwanjani hadi sasa.
Taarifa zinadai kwamba mchezaji huyo baada ya kusumbuliwa na maumivu ya nyama za paja alikaa sawa na kuanza mazoezi mepesi akijiandaa na mchezo dhidi ya Tanzania Prisons (Mei 9) lakini alijikuta akijitonesha tena na kukaa nje ya uwanja hadi sasa na huenda akaomba kuondoka Yanga.