Kama ulidhani wanapata tu ushindi nyumbani wakicheza kwenye Uwanja wa Nyankumbu mkoani Geita basi subiri uone kwani Geita Gold wamesema wanataka pointi tatu dhidi ya Simba leo kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Geita Gold haijapoteza mchezo wa nyumbani iliocheza kwenye Uwanja wa Nyankumbu mkoani Geita msimu huu ila imepoteza mchezo mmoja tu wa nyumbani dhidi ya Yanga ambao ulipigwa nje ya Geita ukichezwa CCM Kirumba, Mwanza.
Kesho Geita Gold itaikaribisha Simba katika uwanja huo saa 10 jioni huku Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Mathias Wandiba ‘Master’ akitamba kuwa wachezaji wake wako kamili wameandaliwa vizuri kimbinu, kiufundi na kisaikolojia kuukabili mchezo huo na kubeba pointi tatu mbele ya mnyama.
Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari jijini hapa jana, Wandiba amesema malengo yao ni kupata alama tatu na kuendelea kuvhanja Mbuga kwenye nafasi za juu ili kutimiza malengo ya klabu hiyo.
“Tumefanya maandalizi yetu ya mwisho kuelekea mchezo huu wachezaji wako sawa tunacheza mechi kubwa na timu kubwa lakini tumejiandaa target yetu ni kufika kwenye malengo yaliyokusudiwa,” amesema Wandiba na kuongeza
“Simba ni bora lakini tuna wachezaji imara, vijana na waliojiandaa kupambana kiufundi wako vyema tumewaandaa vizuri kimbinu, kisaikolojia wachezaji wetu wote 26 wako vizuri hakuna majeruhi wote wako timamu, timu bora ndiyo itakayoshinda,” amesema.
Nyota wa timu hiyo, Maka Edward amesema bila hata kukumbushwa wachezaji wanafahamu umuhimu wa mchezo huo na wanautaka ili kuzidi kujiongezea sifa hivyo wana morali na ari kubwa ya kupambana leo dhidi ya mnyama na kupata alama tatu.
“Wachezaji tumejiandaa vizuri tuko timamu kiakili na kimwili tumejiandaa kushinda kesho, tukiyafuata waliyotuelekeza walimu kwa asilimia 100 basi tutashinda, ni mchezo mzuri kila mchezaji anauhitaji morali iko juu njia sahihi ni kufuata maelekezo ya walimu ili tusipoteze nyumbani,” amesema Maka.