KIUNGO fundi wa Simba anayekipiga Mtibwa Sugar kwa mkopo, Said Ndemla huenda msimu ujao akaitumikia Azam FC kutokana na matajiri hao wa Dar es Salaam kuanza kumnyatia kimya kimya.
Wakati wanasaka saini ya Ndemla, imedaiwa kuwa mabosi wa Azam watatema mastaa wao kibao akiwamo Frank Domayo ambaye mkataba wake unamalizika Mei 30 mwaka huu, Idrisa Mbombo, Yvany Mbala, kipa Mathias Kigonya na Never Tigere.
Ndemla aliyeitumikia Simba tangu mwaka 2013 bila kutoka, katika dirisha dogo la Januari alitolewa kwa mkopo wa miezi sita kwenda Mtibwa anapocheza kwa kiwango kikubwa hadi sasa jambo lililowavutia mabosi wa Azam.
Gazeti la Mwanaspoti limemnukuu mmoja wa viongozi wa ndani ya Azam (jina lake kapuni), na kueleza kuwa msimu huu utakapomalizika watasafisha kikosi chao kwa kuondoa wachezaji kadhaa na kusajili wapya miongoni mwao akiwamo Ndelma.
“Kuna wachezaji wataondoka mwisho wa msimu, tumeanza taratibu kufanya ‘scouting’ ya watakaoziba nafasi hizo na Ndemla ni miongoni mwa wachezaji wanaotazamwa kwa karibu na kama mambo yataendelea kuwa hivi basi tutamsajili,” alisema kigogo huyo na kuongeza;
“Hakuna mazungumzo rasmi yaliyofanyika lakini nikuhakikishie tu kwa Tanzania ukizitoa Simba na Yanga hakuna mchezaji atakataa kujiunga na Azam.”
Alipotafutwa Ndemla kulizungumzia hilo, hakuwa tayari kusema chochote na kueleza kuwa kwa sasa anaipambania Mtibwa kuhakikisha inafikia malengo yake. “Achana na habari hizo kwanza, kwa sasa nipo Mtibwa kuhakikisha timu inafikia malengo,” alisema.
Credit: MwanaSpoti.