Wachezaji Kibwana Shomari wa Yanga na Kibu Denis wa Simba wamelazimika kukimbizwa hospitali baada ya kupata majeraha katika mchezo wa Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).
Wachezaji hao wamepata majeraha baada ya kugongana vichwa dakika ya 62 wakiwania mpira wa krosi uliyopigwa na Pappe Sakho.
Baada ya kuanguka Kibwana alionekana kuzidiwa huku akivuja damu kichwani na kukimbizwa kwenye gari la huduma ya kwanza huku baada ya mashauriano ya madaktari wa Yanga na wale wa huduma ya kwanza mchezaji huyo akakimbizwa hospitali kwa matibabu zaidi.
Baada ya tukio hilo Kibu Denis aliendelea na mchezo lakini hakudumu baada ya kuamua kukaa chini dakika ya 74 kisha benchi la ufundi la Simba kumfanyia mabadiliko na nafasi yake kuchukuliwa na Yusuph Mhilu.
Muda kidogo baada ya mabadiliko hayo, Kibu naye alipandishwa kwenye gari la huduma ya kwanza naye kuwahishwa hospitalini.
Ilipofika dakika ya 86 beki wa kulia Jimmyson Mwanuke naye alishindwa kuendelea na mchezo baada ya kugongana na Fiston Mayele na kutolewa nje huku nafasi yake ikichukuliwa na Erasto Nyoni.
Mchezo huo umemalizika dakika 90 kwa Yanga kuibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Feisal Salum dakika ya 25 ni rasmi sasa Yanga anasubiria mshindi kati ya Coastal Union dhidi ya Azam kucheza naye fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).