Home Habari za michezo MASAA KADHAA KABLA YA KUIVAA YANGA…PABLO ‘AWASUSIA WACHEZAJI MECHI’…AFICHUA ALICHOWAELEZA..

MASAA KADHAA KABLA YA KUIVAA YANGA…PABLO ‘AWASUSIA WACHEZAJI MECHI’…AFICHUA ALICHOWAELEZA..


Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ Simba SC, Pablo Franco amekiri kuwa wapinzani wao, Young Africans wataingia kwenye mchezo wa leo Jumamosi (Mei 28) wakiwa kwenye kiwango bora zaidi yao, lakini kikosi chake kimejiandaa vya kutosha kuwasimamisha.

Timu hizo zitakutana Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kwenye mchezo wa Nusu Fainali ya ‘ASFC’ kuanzia saa 9:30 alasiri, huku kila mmoja akihitaji kutinga Fainali na baadae kutawazwa kuwa Bingwa wa michuano hiyo kwa msimu huu 2021/22.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Ijumaa (Mei 27), Kocha huyo kutoka nchini Hispania amesema, anatambua ubora wa kikosi cha Young Africans, hivyo alijitengea muda wa kufahamu mbinu zao kupitia vyanzo vyake mbalimbali.

Amesema mbali na yeye kuichunguza Young Africans, pia anafahamu Benchi la ufundi la wapinzani wao lilitenga muda kuifuatilia Simba SC katika michezo yake ya hivi karibuni, hivyo anatarajia kesho mchezo utakua na ushindani wa hali ya juu.

“Kama ambavyo wenzetu walitenga muda wa kutufuatilia na kuja kuangalia mechi zetu nasi tumefanya jambo kama hilo ili kuona namna gani tunacheza mechi hiyo kwa ubora dhidi yao ili kupata ushindi,”

“Mechi iliyopita dhidi ya Yanga na nyingine zilizofuata maandalizi na mbinu tutakazotumia kwenye mechi hiyo itakuwa tofauti kabisa ili kuona tunakuwa bora zaidi ya Mpinzani”

“Katika mazoezi yetu ya wakati huu tunafanya yale tuliyokuwa na mapungufu nayo ili kuwa bora pamoja na namna gani tutakwenda kuwazuia wapinzani kutokana na uimara wao na namna gani tutakwenda kuwashambulia kutokana na mapungufu yao”

“Wachezaji wangu huu mechi ipo mikononi mwao wao wana kila sababu ya kupambana na kuhakikisha Simba inafikia malengo yake ya kupata ushindi na kusonga kwenye hatua inayofuata. Tupo karibu na kutetea taji hili wachezaji mbali ya mazoezi huwa nazungumza nao mmoja kwa mmoja.” Amesema Kocha Pablo.

Mshindi wa mchezo huo atacheza na mshindi wa mchezo wa Nusu Fainali ya Pili itakayounguruma keshokutwa Jumapili (Mei 29) jijini Arusha katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, kati ya Azam FC ya Dar es salaam dhidi ya Coastal Union ya Tanga.

SOMA NA HII  KAIZER CHIEF WAGOMEA MASHARTI YA NABI....KUMBE ALITAKA KUWACHUKUA MAKOCHA WOTE YANGA...