Home Habari za michezo KUMWEMBE: SIMBA KUZIFUNGA ZILIZOFIKA FAINAL CAF HAIMAANISHI KWAMBA NI TIMU BORA…

KUMWEMBE: SIMBA KUZIFUNGA ZILIZOFIKA FAINAL CAF HAIMAANISHI KWAMBA NI TIMU BORA…


KWAMBA klabu mbili za Berkane na Orlando Pirates zilifungwa pale Temeke na Simba na sasa timu hizi zimefika fainali ya kombe la Shirikisho, hii maana yake nini? Nimesikia mitaani watu wakiwa na mikanganyiko ya hoja ambayo haina maana.

Kuna wanaodai kwamba Simba ilizifunga timu bora ambazo zimefika fainali kwahiyo na yenyewe ni bora. Ni kweli Simba ni bora lakini pambano moja la soka haliamui mlinganisho wa ubora kati ya timu moja na nyingine. Kitu cha msingi ni mwendelezo wa ubora. Msimu huu tu Simba ilifungwa na Mbeya City na Kagera ndani ya siku kumi.

 Haizifanyi timu hizi kubwa bora mbele ya Simba. Ni matokeo fulani ya dakika 90 tu lakini katika soka letu kwa ujumla wake Simba huwa inalinganishwa na timu moja tu, Yanga. Hata Azam hawapo katika kundi la watu hawa wawili. Simba inaweza kufungwa na Azam au Polisi Tanzania lakini ubora wa Simba upo palepale.

Berkane, licha ya fitina nyingi za soka la Afrika lakini mwaka 2020 walichukua Kombe la Shirikisho. Mwaka mmoja kabla ya hapo yaani 2019 walifika fainali dhidi ya Zamalek. Utashangaa nini kwao kufika fainali za mwaka huu hata kama walifungwa na Simba Uwanja wa Mkapa? Kumbe wao wanaviwango vyao na haishangazi wakifika walipofika. 

Hawa rafiki zetu Orlando Pirates wamewahi kuchukua ubingwa wa Afrika na juzi juzi tu wamewahi kucheza fainali. Kwao kutinga fainali za Shirikisho sidhani kama ni jambo la ajabu zaidi. Kuna viwango wamejiwekea kabla ya hapo ambavyo sisi hatuna.

Nawashukuru Simba wameanza kuzoea kucheza makundi. Kwa sasa hiki ni kiwango chao. Natazamia warudi tena hapo mwakani halafu kisha tena na tena. Wanaweza pia kwenda nusu na hivyo kujiweka katika viwango vya makundi na nusu fainali. Hiki ndicho ambacho kinatakiwa kuliko kuhukumu mambo kwa pambano moja tu la soka.

Leo Simba wakienda nusu fainali hauwezi kushangaa sana kwa sababu tayari wameshacheza makundi kwa mfululizo. Mpira una viwango vyake. Na hata ukitazama, hata kama Yanga atatwaa ubingwa msimu huu huku wakicheza soka zuri lakini Simba wapo mbele yao kwa hatua kadhaa. Angalia jinsi ambavyo Yanga walitolewa kirahisi na Rivers United.

Tatizo kubwa la Yanga na Simba ni kuacha pengo kubwa la mafanikio dhidi ya wakubwa wengine. Fikiria jinsi ambavyo mara ya mwisho Simba kufika nusu fainali ya klabu ya Afrika ilikuwa mwaka 1974. Inakaribia miaka 50 sasa. Na ndio timu pekee ambayo imewahi kufika hatua kubwa kama hiyo kutoka Tanzania.

Yanga ilifika hatua kubwa zaidi katika michuano hiyo mwaka 1998 wakati walipotinga robo fainali. Hawajawahi kurudi huko. Wanasema ukishika pesa inaweza kukuzoea. Ukiwa unafanya kazi katika duka la manukato unaweza kujikuta unanukia kila nyakati. Harufu ya mafanikio katika michuano ya kimataifa haijawakaa vyema Simba na Yanga. Waangalie hawa TP Mazembe. Misimu miwili hii wana timu mbovu lakini tayari mwaka huu wamefika hatua ya nusu fainali ya michuano ya Shirikisho. Wao wana harufu ya michuano hii kuliko Simba na Yanga. Na bado naamini kikosi hiki cha Mazembe sio kikali kuliko Simba. Wakati mwingine historia inasaidia.

SOMA NA HII  CHEZA SLOTI YA SWEET BONANZA 1000 KASINO! USHINDI X25,000 YA DAU LAKO...

Ni kama vile ambavyo hatutashangaa msimu ujao Mamelodi Sundowns wakachukua ubingwa wa Afrika licha ya msimu huu kupigwa ngumi ya pua katika robo fainali na Petro Atletico ya Angola. Unajua tu kwamba mwaka huu wameteleza lakini wao viwango vyao ni nusu fainali na fainali au ubingwa. Ndivyo wakubwa walivyo.

Al Ahly hachukui ubingwa kila msimu, lakini wote tunafahamu kwamba kiwango chake ni kuanzia nusu fainali hadi ubingwa. Hivi ndivyo viwango ambavyo timu zetu hazijajiwekea lakini tumeanza kujisifu au kupima ubora wetu kwa takwimu za kuwafunga ambao wamekwenda fainali. Sio sawa.

Lakini hapohapo katika suala la viwango tujikumbushe kwamba kuna viwango vya klabu na viwango vya nchi. Hao Berkane Uarabu wao tu unawabeba. Historia ya nchi yao tu katika michuano hii inawabeba. Taifa ambalo Waydad na Raja wamekuwa wakifanya hivi kwa muda mrefu itashangaza nini kama Berkane ikifika fainali. Unajua tu kwamba Wamorroco ni wazuri hata wakitumia wachezaji wa ndani.

Kitendo cha Simba kuwafunga Berka-ne na Orlando pale Temeke kisha wao wakaenda fainali kisitulemaze. Wenzetu wameweka viwango vyao kwa muda mrefu. Ni kama tu timu ya kawaida ikimfunga Yanga au Simba katika ligi. Na wakati mwingine kupitia fitina za mpira wa Afrika inakuwa rahisi kupata ushindi wa mechi moja lakini kwa ujumla wake haimaanishi kwamba mpira wenu umekua.

Mwisho wa siku lazima tujikumbushe kama hawa wanaofika fainali wana vigezo ndani na nje ya uwanja. Kiukweli wanaweza kuwa wanateleza wakati fulani lakini timu zao zimeundwa kimpira hasa kuliko timu zetu. Uwekezaji wao ni mkubwa hasa. Hizi ndizo timu ambazo zinanunua wachezaji kwa bei mbaya. Zina viwanja binafsi vya kisasa kuanzia vile vya mazoezi hadi vya mechi. 

Zinaajiri makocha wa bei mbaya. Vitu vyote hivi ni tofauti na sisi. Kwa kuanzia tu wachezaji wetu wa kigeni wengi ni wale wa uhamisho huru (free transfer). Hatujawahi kumpata mchezaji wa dola laki mbili mpaka sasa. Sawa, tunaweza kubahatisha kupenya huku na kule pamoja na kuwafunga wakubwa katika Uwanja wa Mkapa pale Temeke, lakini kwa ujumla wake viwango vyao na vyetu ni vitu viwili tofauti. Sisi tunategemea hamasa zaidi kuliko uwekezaji. 

Ifike mahala kwamba Simba isipotinga hatua ya robo fainali basi Afrika nzima inashangaa. Huo ndio mwanzo mzuri wa ukuaji wa viwango vyetu. Hapa miaka ya karibuni tayari watu wengi wa Afrika wameanza kuiamini katika muktadha huo.

Rafiki zangu Yanga wao ndio wana safari ndefu zaidi ya kurudisha daraja lao katika michuano ya Afrika. Kama wakichukua ubingwa msimu huu na kushiriki michuano ya Afrika msimu ujao wakumbuke kwamba kuna viwango inabidi waviweke na kuviendeleza karibu kila mwaka kama ambavyo Simba imefanya miaka ya karibuni.