Ni zamu ya mashabiki wa Yanga kutamba kila kona, kutokana na timu hiyo kubakiza mechi moja tu kutangaza ubingwa msimu huu.
Yanga inaongoza kileleni kwa pointi 64, ikishinda mchezo mmoja kati ya minne iliyobakia itafikisha pointi 68 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote, kwani mtani wake wa jadi Simba ana 51 na akishinda mechi tano zilizobakia itafikisha 66.
Uhakika wa ubingwa huo kwa Yanga, umemfanya shabiki kindakindaki wa timu hiyo anayetambulika kwa jina la Anwari Mwita Wambura ‘Yanga Kigelegele’ kujimwambafai.
“Mtaani tunasikika Yanga tu wenzetu wapo wapi? wamepoa kama vile wamehama nchini, jamani jamani Yanga ni tamu hii,” amesema Yanga Kigelege na ameongeza;
“Mchezo huu hauhitaji makasiriko, raha ya kigelegele ukikipiga angalau uitikiwe na majirani zako, hii ndio Yanga ya mataji bhana.
Shabiki mwingine anayejulikana kama Jesca Manji, amesema ni mwaka wa rangi za kijani na njano kutamba kila kona, huku akiwataka majirani zao (Simba) wapumzike.
“Sikuona timu ya kuizuia Yanga kunyakua mataji ya Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho Azam (ASFC), ina kikosi kizuri, huu ni mwaka wa wetu wa kutamba,”amesema.
Justin Joel ambaye ni shabiki wa Simba lialia na mtendaji mkuu wa tawi la Wekundu wa Msimbazi, amejibu mapigo akiwaambia watani wao, wakutane kimataifa. “Tukutane michuano ya CAF ambako kutaonyesha ukomavu wa kila timu na uzuri hatujabebwa na timu yoyote kucheza michuano hiyo kwa mwaka huu, hivyo Wanasimba hatuna sababu ya kutembea kinyonge,” amesema.