Home Habari za michezo KUTANA NA YOHANA MWONGA…MLEMAVU WA MACHO ANAYETAMANI KUIONA SIMBA ‘LIVE’…AMZIMIKIA BARBARA GONZALEZ…

KUTANA NA YOHANA MWONGA…MLEMAVU WA MACHO ANAYETAMANI KUIONA SIMBA ‘LIVE’…AMZIMIKIA BARBARA GONZALEZ…

 


“NATAMANI siku moja niione familia yangu na wachezaji wa Simba kwa macho.” Hiyo ni kauli ya mdau na shabiki wa soka jijini Mbeya, Yohana Mwonga ambaye ni mlemavu wa macho kwa miaka 34 sasa hajaona jua.

Mwonga ambaye ni mkazi wa Galijembe katika Kata ya Tembela wilayani Mbeya amekuwa maarufu sana kwa wadau wa michezo jijini Mbeya kufuatia mchango wake katika medani za soka.

Mwanaspoti lilimtafuta Mwonga ambaye alieleza hisia zake za kutamani kumuona kwa sura japo kwa dakika moja mke na watoto wake, lakini akitaka pia kuwaona nyota wa Simba.

ALIPATAJE UPOFU

Mwonga anasema hakuzaliwa na ulemavu huo, isipokuwa ni ugonjwa ambao aliupata kwa njia ambazo haelewi hadi leo, kwani alianza kuona mabadiliko mwaka 1988 alipokuwa darasa la sita na alikuwa vizuri kwenye masomo yake.

Anasema hata baada ya kupatwa na tatizo hilo alipelekwa katika Shule ya Wasioona ya Katumbambili iliyopo wilayani Rungwe mkoani Mbeya ambapo alifanya kweli katika masomo.

“Sikuzaliwa hivi, bado huwa najiuliza tatizo lilitoka wapi. Darasani nilikuwa nafanya vizuri hadi nilipopelekwa shule ya wasioona bado niliwasumbua wenzangu kwa kuwa wa kwanza hadi kuvushwa madarasa mawili na nikashinda mtihani wa darasa la saba,” anasema Mwonga ambaye alipata ufaulu wa daraja la pili katika mtihani wa kidato cha nne, lakini kumpoteza mama yake aliyekuwa nguzo ilisababisha ashindwe kuendelea na masomo ya elimu ya juu.

HAIJUI SURA YA MKE WAKE

Mwanachama huyo wa Simba anasema kwa miaka zaidi ya 10 aliyonayo kwenye familia, lakini hamjui mke wake kwa sura wala watoto wake japokuwa anashukuru maisha yanaenda vizuri.

Anasema siku ikitokea akapata muujiza wa Mungu kumuamsha akaona, anatamani kumuona mke wake anafananaje kwa sura na hata watoto wake wakoje.

“Mke wangu simjui anafananaje sura yake, hata watoto wangu pia. Huwa naomba sana Mungu siku akinifungua macho yangu niione familia yangu, lakini pia niione Simba yangu,” anasema Mwonga.

“Nasikia redioni wakitajwa Aisha Manula, Mohamed Hussein, Clatous Chama na Benard Morrison natamani kuwaona kwa macho hawa wachezaji lakini hata Barbara Gonzalez (mtendaji mkuu Simba) nimuone yukoje.”

Anaongeza kuwa siku akikutana na viongozi wa Simba atawaeleza nia na mapenzi yake kwa timu hiyo, akiomba kukutana na wachezaji ili kuandika historia ya maisha.

ANAFANYAJE KAZI ZA SOKA

Mkereketwa huyo wa Simba anakiri kuwa na wakati mgumu katika kutekeleza majukumu yake uwanjani, akibainisha kuwa yapo matukio ambayo hulazimika kuomba kusaidiwa.

Anasema anapopewa jukumu la kusimamia mechi, huomba msaada wa kuwa na msaidizi wa karibu ambaye atakuwa akifuatilia matukio ya ndani ya uwanja.

“Kama ni kufanya mabadiliko situmii ubao, bali nitamuita refa kwa sauti kuashiria kufanyika ‘sub’ na kama kuna tatizo lingine viongozi wa timu watakuja nilipo na kuniambia kwa sauti,” anasema Mwonga.

ALIVYOINGIA KWENYE SOKA

Mwonga anasema kuwa kabla ya kupatwa na tatizo la macho, alikuwa mchezaji mzuri ambaye alikuwa na matarajio makubwa ya kufika mbali japokuwa yaliyotokea anamuachia Mungu.

SOMA NA HII  FEI TOTO ATAJA KIKOSI BORA CHA MSIMU...AMTAJA POCOME...CHAMA NJE

Anasema katika miaka ya nyuma akiwa mzima wa macho alikuwa akicheza soka la kuvutia akimudu nafasi za beki na winga, na shughuli yake haikuwa ya kitoto uwanjani.

Anasema kwa sasa akisikiliza kazi za wachezaji wa kipindi hiki anajifananisha na winga wa zamani wa Mtibwa Sugar na Simba, ambaye kwa sasa anakipiga Namungo, Shiza Kichuya na Mohammed Hussein ‘Tshabhalala’. “Mipira yangu ya kona ilikuwa haiguswi na mtu, inaenda moja kwa moja wavuni, lakini hata ile kazi ya kudhibiti mipira kwa adui anayofanya Tshabhalala, Kapombe na Inonga inanikumbusha enzi zangu,” anasema mdau huyo.

ANACHOFANYA KWA SASA

Mwonga anasema kutokana na matatizo aliyonayo kwa sasa hana kazi kwani miaka ya nyuma alikuwa akijikongoja kufanya shughuli za kilimo, lakini kwa sasa mkewe ndiye amebaki shambani.

Anasema anachopambania ni kuwa karibu na familia akisaidia shughuli ndogondogo zilizo ndani ya uwezo wake, japokuwa kuna wakati hali inakuwa mbaya hasa kiuchumi.

“Kwa ujumla siwezi kukaa barabarani kama wengine kuomba msaada, ila kama kuna ndugu, jamaa au rafiki zangu nikikwama huwa naomba. Kuna wakati hali inakuwa ngumu sana,” anasema.

AJIVUNIA KUZALISHA WACHEZAJI

Mwonga anasema licha ya matatizo aliyonayo, lakini anajivunia kupitia ndondo alizokuwa anasimamia wametoka wachezaji wengi ambao kwa sasa wanacheza soka la ushindani.

Anasema kama haitoshi kupitia kipaji chake cha uhamasishaji amefanikiwa kuipandisha timu ya Mbeya Kwanza katika Ligi Kuu Bara na kwamba ndio timu ambayo hadi sasa anaishabikia kwa Mkoa wa Mbeya.

Mwonga anasema kama haitoshi ameweza kuanzisha timu ya wasichana japokuwa kutokana na uwezo mdogo kiuchumi ameshindwa kuiendesha, huku akiomba wadau na mashabiki wenye nia waweze kumsaidia kuiimarisha timu hiyo.

“Wapo wachezaji ambao walikuwa kwenye timu zetu za ndondo huko vijijini kama Oscar Mwajanga wa Mbeya Kwanza, lakini hata timu hiyo nilikuwa kwenye kamati ya uhamasishaji na tumefanikiwa kuipandisha Ligi Kuu,” anasema Mwonga.

Anasema kuwa ni nadra kutokuwapo kwenye mechi hasa pale Mbeya Kwanza inapocheza katika Uwanja wa Sokoine, huku akieleza kuwa anatamani kushuhudia mchezo baina ya Mbeya Kwanza na Simba.

AOMBA MSAADA

Mpenzi huyo wa soka ambaye huhudhuria sana uwanjani, anasema kutokana na gharama za maisha kupanda hujikuta katika wakati mgumu ambao muda mwingine watoto wake hukosa huduma shuleni.

Anasema pamoja na kupambana kushirikiana na mkewe, lakini kwa sasa watoto wake wanaosoma shule ya msingi hawana sare.

Mwonga anasema kwa mtu mwenye uwezo na nia njema anaomba kusaidiwa hata vifaa vya shule ili watoto waendelee kupata haki yao ya elimu kwa maisha yao ya baadaye.

“Kuna muda wanakuja wanalia kwamba wamepigwa hawana sare za michezo, lakini naenda shuleni kuomba wawasamehe niendelee kutafuta, niombe wenye uwezo wanisaidie,” anasema Mwonga.

Credit:- MwanaSpoti.