KOCHA Mkuu wa Geita Gold, Fred Felix Minziro amefunguka kinachombeba straika wa timu hiyo, George Mpole msimu huu hadi kuwa kipenzi cha mashabiki.
Minziro amesema kama kuna jambo amekuwa akimsisitiza mara kwa mara nyota huyo wa Taifa Stars, ni kujua mashabiki wanampenda, hivyo asiyumbe ili asitoke kwenye mstari.
“Nidhamu, utulivu na juhudi vinambeba kuanzia mazoezini hadi uwanjani kwenye mechi na ana uwezo wa kufunga awapo eneo la kufunga. Pamoja na kuzungumziwa sana, bado ana utulivu na anajua kazi haijaisha na anapenda kujifunza kila wakati,” alisema na kuongeza;
“Tanzania ina vipaji vingi, hata hivyo wengi nidhamu ndiyo inawaangusha na kupoteza viwango vyao.”
Kuhusu Mpole kuitwa Taifa Stars, alisema; “Akiitwa Stars, tunazungumza na namsisitiza nidhamu na kujua Kocha Kim Poulsen anahitaji nini kutoka kwake, hivyo najisikia faraja kufunga bao dhidi ya Niger. Pia anajifunza mengi kutoka kwa wenzake waliofanikiwa.”
Kwa upande wa Mpole alisema; “Kocha ananijenga kiakili na kufikiria mbele zaidi kuliko kulewa sifa, kubwa zaidi ni ushirikiano kutoka kwa wachezaji wenzangu.”
Mpole hadi sasa ana mabao 14 Ligi Kuu Bara sawa na Fiston Mayele wa Yanga na amekuwa na kiwango bora msimu huu.
Minziro, pia alizungumzia Ligi Kuu Bara kwa jumla na kuzitaja Yanga na Simba zimeshamaliza ligi huku akifichua kazi kubwa imebaki kwenye kushuka daraja na nafasi ya tatu na nne.
“Taswira ya ushindani msimu huu, inaonyesha namna msimu ujao utakavyokuwa mgumu na timu zinapaswa kusajili vizuri, hadi sasa hujui nani anashuka,” alisema.