KIUNGO mshambuliaji wa Asec Mimosas ya nchini Ivory Coast, Stephane Aziz Ki, huenda akavunja rekodi ya usajili ya beki wa kulia wa timu hiyo, Djuma Shaaban.
Nyota huyo raia wa Burkina Faso inaelezwa yupo nchini Tanzania akiwa amefichwa na mabosi wa Yanga kwenye moja ya hoteli kubwa jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kufanya mazungumzo ya kusaini mkataba.
Djuma ndiye mchezaji anayeongoza katika dau kubwa la usajili katika msimu uliopita baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili wenye thamani ya Sh 500Mil.
Taarifa kutoka ndani ya Yanga, zinasema kiungo huyo yupo nchini na amefikia katika moja ya hoteli kubwa iliyopo Posta jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kufanya mazungumzo ya kutua Jangwani.
Mtoa taarifa huyo alisema kuwa kiungo huyo alianza muda mrefu mazungumzo na Yanga kwa muda wa wiki mbili zilizopita kabla ya juzi Jumatano kutua nchini kimyakimya kwa ajili ya kufikia muafaka mzuri wa kusaini mkataba wa miaka miwili wenye thamani ya Sh 500Mil, wenye kipengele cha kuongeza mwaka mwingine mara baada ya mkataba wa awali kumalizika.
Aliongeza kuwa kiungo huyo anaweza kuweka rekodi kubwa ya usajili ndani ya misimu miwili iliyopita kutokana na dau kubwa analohitaji linalofikia zaidi ya Sh 500Mil kwa misimu miwili.
Kiungo huyo pia mkataba wake unajumuisha tiketi ya daraja la kwanza ya ndege itakayokuwa inampeleka na kumrudisha kutoka kwao Burkina Faso atakapokuwa katika mapumziko au dharura. Pia atapewa nyumba na gari binafsi la kutembelea.
“Djuma (Shaaban) ndiye mchezaji mwenye rekodi ya usajili ambaye yeye dau lake la usajili lilifikia Sh 500Mil ambalo huenda likavunjwa katika msimu huu na Ki kama Yanga wakifikia muafaka mzuri.
“Kwani tayari yupo nchini baada ya viongozi kumleta kwa ajili ya kufanikisha usajili wake kwa ajili ya msimu ujao ambao tutacheza Ligi ya Mabingwa Afrika. Hivyo kama ataikubali ofa aliyowekewa na mabosi wa Yanga, basi atasaini mkataba.
“Hivyo ni lazima tufanye usajili bora utakaoendana na hadhi ya michuano hiyo, Ki yupo nchini tayari kwa ajili ya kukamilisha dili hilo la usajili,” alisema mtoa taarifa huyo.
Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela, alipotafutwa alisema: “Wapo wachezaji wengi tulio katika mazungumzo na yeye Ki huenda akawa kati ya wachezaji hao, hivyo hilo ni suala la muda, tusubirie kila kitu tutakiweka wazi hivi karibuni.”