Inaweza kuwa habari ya kushtua sana kwa mashabiki wa Yanga, lakini ndivyo ilivyo kwamba wakala wa Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi, alilipelekea jina la kocha huyo kwa mabosi wa Simba ili kumtafutia kazi mpya.
Za Ndaani Kabisa, zinasema kuwa wakala huyo alilipelekea jina la Nabi kwa vigogo wa Msimbazi, baada ya awali klabu hiyo kuchomoa kumchukua ilipokuwa ikisaka kocha wa kuziba nafasi ya Sven Vandenbroeck aliyekuwa ametangaza kuachia ngazi siku chache baada ya kuifikisha timu hiyo makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita.
Taarifa hizo zinasema Simba ilimkataa Nabi na kumchukua Didier Gomes aliyekuwa amepishana na Nabi ndani ya El Merreikh ya Sudan.
Gomes alijiondoa El Merreikh ilipotinga makundi na nafasi yake kuchukuliwa na Nabi ambaye alikaa kwa muda mchache kabla ya kufurushwa baada ya kuboronga makundi ikiwamo kutoka suluhu na Simba mjini Khartoom katika mechi zao za makundi msimu huo.
Inadaiwa kufanya vyema kwake akiwa na Yanga, kulimfanya wakala wa Nabi kuwarudia tena Simba ilipomtema Pablo Franco aliyekuwa ameziba nafasi ya Gomes, huku jeuri ya kuwapigia simu mabosi wa Wekundu ikitokana na mkataba wa mteja wake Yanga kuwa ukingoni.
Hata hivyo, Za Ndaani zinasema, mabosi wa Simba wameamua kumkaushia Nabi kuhofia wasizinguane na wenzao wa Yanga, pia msimamo wa Nabi wa kutaka kusalia Jangwani ili kuendeleza kile alichoanza nacho tangu ajiunge nayo Aprili mwaka jana, ndio imewatia ubaridi vigogo wa Msimbazi. Mkataba wa Nabi unatrajiwa kumalizika Oktoba mwaka huu.
Nabi tangu ajiunge na Yanga, ameiongoza Yanga katika mechi za Ligi Kuu Bara 34, ameiongoza Yanga kucheza mechi 33 mfululizo bila kupoteza, ukiacha mchezo mmoja aliokuwa jukwaani siku ya kwanza ya kazi yake, timu hiyo ilipolala kwa Azam Aprili 25, 2021.