Aliyekuwa nyota wa Yanga, Saidi Ntibanzokiza ‘Saido’ jana aliondoka nchini kurudi kwao Burundi huku akiokeza kuwa atarudi Bongo msimu ujao.
Saido aliyemaliza mkataba na Yanga, Jumapili hii alitinga kambini kuwaaga wachezaji wenzake pamoja na benchi la ufundi na jana mchana alipanda ndege kwenda kwao, lakini akafunguka kuwa atarudi tena nchini.
Nyota huyo aliyeifungia Yanga mabao saba na kutoa asisti nne, ameeleza kuwa hatarudi Yanga, lakini msimu ujao atakuwa Tanzania.
“Naenda nyumbani kupumzika lakini nitarudi Bongo Mungu akijaalia. Sitarudi Yanga ila nitabaki kuiheshimu kutokana na nyakati tulizokuwa pamoja,” alisema.
Ifahamike kuwa Saido anawindwa na timu tatu hadi sasa zikiongozwa na Simba ambayo tayari imeanza mazungumzo naye na ameipa masharti na vigezo anavyotaka ili asaini, sambamba na Azam na Singida Big Stars (zamani DTB). Alipoulizwa kuhusu ni timu gani kati ya hizo atarudi msimu ujao kucheza, aliweka wazi kuwa hadi sasa hajafikia mwafaka na timu yoyote lakini anaamini siku sio nyingi atasaini mkataba mpya.
“Timu zote hizo ni nzuri na baadhi tumezungumza nazo lakini sijasaini. Ni mambo madogomadogo ya kimkataba yamefanya nisisaini na kama yakitimizwa basi nitasaini Inshallah,” alisema, lakini inafahamika kuwa amefanya mazungumzo na Simba na kuwapa masharti ya mkataba wa mwaka mmoja ambao utakuwa na kipengele cha muda mwingi wa kucheza na kuondoka akipata timu.