Wakati mabosi wa Simba SC wakitajwa kuwa kwenye mazungumzo na mtaalamu wa viungo ili aweze kuibuka ndani ya kikosi hicho ambaye ni Adel Zraine, vigogo wengine nao wamemvutia kasi kocha huyo.
Zraine aliwahi kuwa ndani ya kikosi cha Simba SC na alifungashiwa virago baada ya timu hiyo kuondolewa katika hatua ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu wa 2021/22.
Taarifa zimeeleza kuwa wakati Simba SC wakiwa kwenye hesabu za kumrejesha kocha huyo Tanzania, Azam FC wameweza kumfuata ili aweze kujiunga na timu hiyo.
“Simba SC wakichelewa dili litakuwa gumu kwao kwa kuwa tayari Azam FC wameanza mazungumzo na Adel, (Zraine) ili kuweza kupata saini yake kwa msimu ujao,” ilieleza taarifa hiyo.
Zraine kwa sasa anatimiza majukumu yake ndani ya Klabu ya Al Wehdat ya nchini Jordan anafanya kazi na Didier Gomes Da Rosa ambaye alikuwa naye pamoja ndani ya kikosi cha Simba SC.
Zraine aliweza kuweka wazi kuwa anaipenda Tanzania kwa kuwa alifanya kazi kwa upendo.
“Ninaipenda Tanzania ni nchi ambayo inapenda mpira na watu wake ni wakarimu kama itatokea ninaweza kurudi lakini siwezi kusema ni timu ipi kwa sasa japo kuna timu kutoka Tanzania inaonyesha nia ya kuhitaji nirudi,” alisema.