BAADA ya kumalizana na Moses Phiri kutoka Zanaco ya Zambia ikimpa mkataba wa kuitumikia Simba, mabosi wa timu hiyo hawajalala kwani wamenasa mashine nyingine mpya kwa ajili ya msimu ujao.
Usiku wa Jumamosi mabosi hao walipambana na kufanikiwa kunasa saini ya Habib Kyombo kutokea Mbeya Kwanza aliyojiunga nayo dirisha dogo la usajili akitokea TS Sporting ya Afrika Kusini.
Chanzo cha habari kilisema kuwa baada ya mvutano wa muda mrefu kwenye kikao cha kukubaliana masuala ya kimaslahi Kyombo akiwa na wasimamizi wake pamoja na viongozi wa Simba mwisho wa siku walikubaliana.
Inaelezwa baada ya mvutano huo Kyombo alikubali kusaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia Simba msimu ujao na sasa atarudi Mbeya Kwanza kumalizia tu michezo iliyobaki Ligi Kuu.
Simba imevutiwa na Kyombo kutokana na uwezo aliouonyesha kwenye ligi amecheza mechi chache ndani ya mkopo wa miezi sita, ila hadi sasa amefunga mabao matano ambayo ni muhimu na kati ya hayo kuna yaliyoipa pointi pamoja na kutoa pasi ya mwisho moja. Simba imedhamiria kuboresha kikosi ili kurudisha makali waliyoyakosa msimu huu ndio maana iliposhindwa kukubaliana kumlipa Kyombo maslahi ya miaka mitatu inaelezwa ikamsainisha miaka miwili.
Inafahamika kuwa Kyombo na uongozi wake kwenye kikao hicho cha kukubaliana kilichofanyika kwa kiongozi mmoja wa juu, walikuwa na hali ya kujiamini katika maslahi kutokana na uwepo wa ofa nyingine mezani ya maana kutoka Singida Big Boys, ila mwisho wa siku mabosi wa Simba walipambana na alinyanyuka kwenye kikao akiwa amesaini miaka miwili.
Ofisa mtendaji mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez alisema masuala yote ya usajili wa wachezaji wapya na wale wanaomaliza mikataba wakishakamilisha wataweka wazi kupitia mitandao yao ya kijamii.
“Tunaendelea na vikao vyetu kuhakikisha tunapata kocha mpya mzuri pamoja na kufanya usajili wa wachezaji wa maana kulingana na mahitaji ya timu yetu. Baada ya kukamilisha haya mawili tutayaweka wazi kama kawaida ya Simba ilivyo,” alisema Barbara na kuwataka mashabiki wa Simba watulie kwani wapo kwenye mapambano ya kuboresha timu ili kurudisha furaha iliyopotea msimu huu.
Naye ofisa mtendaji wa Mbeya Kwanza, Gideon Ngereza alisema akili yao kwa sasa ni kupambana kushinda michezo mitatu iliyobaki ili kumaliza msimu kwenye nafasi nzuri
“Kutokana na hali yetu ilivyo tunahitaji uwepo na uwezo wa mchezaji kama Kyombo ili kutoa mchango kuhakikisha mechi zote tunashinda, ila kutokana na ubora wake ni ngumu kubaki naye kikosini msimu ujao,” alisema Gideon.
“Mezani kwetu tunafahamu kuna timu mbili zinamhitaji ila naamini kuna moja kati ya hizo atakubaliana nayo ila mwenyewe au hiyo timu ndio wanaweza kuweka wazi.”
Kyombo alianza kufahamika katika soka hapa nchini akiwa na kikosi cha Mbao kabla ya kutimkia Singida United ambako nako hakukaa muda mrefu alienda kucheza soka kwenye Ligi Kuu ya Afrika Kusini katika klabu ya Mamelodi Sundowns.
Mamelodi ilimtoa kwa mkopo TS Sporting ya nchini humo kabla ya kumtoa tena kwa mkopo wa miezi sita Mbeya Kwanza na mkataba wake sasa mwisho wa msimu huu unafikia mwisho hivyo Simba inaelezwa imemsajili akiwa huru.