Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) limeifungia Geita Gold FC kusajili wachezaji hadi litakapomlipa aliyekuwa kocha wake Ettiene Ndayiragije.
Katika taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), leo Juni 24, kocha huyo raia wa Burundi alifungua madai dhidi ya Geita Gold FC akidai fidia ya kuvunjiwa mkataba pamoja na malipo mengine wakati akifundisha timu hiyo mkoani Geita.
Kwa mujibu wa taarifa ya FIFA, iwapo Geita Gold FC itakuwa haijamlipa kocha huyo, suala hilo litawasilishwa katika kamati ya nidhamu ya FIFA kwa ajili ya hatua zaidi za kinidhamu.
Aidha, TFF imesema inazikumbusha klabu kuheshimu mikataba ambayo zinaingia na wachezaji pamoja na makocha kwa kuwa ni moja ya vigezo vya kupata leseni ikiwa ni utekelezaji wa kanuni za leseni ya Klabu (Club licensing Regulations)