KOCHA wa Yanga, Nabi Mohammed amewaambia viongozi wafanye kufuru yoyote, winga Simon Msuva akiwashe na Fiston Mayele Jangwani msimu ujao hata kama ni kwa muda mfupi.
Inafahamika kuwa Nabi alipagawa zaidi na Msuva na kuanza kufikiria fomesheni yao baada ya kuangalia mechi ya hisani ya timu Kiba na Samata.
Kwenye mechi hiyo Msuva na Mayele walikuwa timu Kiba na walihusika kwenye bao la dakika ya 15.
Beki wa Azam, Bruce Kangwa alipiga krosi, Mayele akaruka na mabeki wawili wa timu Samatta, kisha mmoja wa mabeki hao kuugonga mpira Msuva akaunasa na kutupia nyavuni bao la kwanza. Bao hilo lilimtingisha Nabi akawaambia viongozi aliokuwa anaangalia nao mechi hotelini; “Mnaonaaa…mnaona mambo yale.”
Habari za uhakika zinasema, kuna mazungumzo mazito yanaendelea baina ya GSM na Msuva na wameweka nguvu kubwa kuhakikisha kila kitu kinamalizika kabla ya wikiendi hii.
Yanga inamshawishi Msuva na zaidi ya Sh350 milioni ili akubali mkataba wao kurejea kuvaa jezi za njano na kijani kwa msimu ujao, usajili ambao pia baadhi ya mastaa wa sasa wa timu hiyo wamekuwa wakishauri kuletwa kwa mshambuliaji huyo mwenye uchu na nyavu.
Yanga inataka kumsajili Msuva kwa muda mfupi aweze kuwaongezea nguvu msimu ujao hasa katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, msukumo mkubwa ukitoka kwa benchi lao la ufundi kwani wamepania kucheza soka la kasi zaidi ya msimu huu na wanaamini Msuva ndiye mtu sahihi kwa Mayele.
Ingawa mabosi wa Yanga wamekuwa wagumu kulizungumzia hilo kwa undani dili hilo mpaka litakapokamilika lakini Nabi ametamka wazi anamtaka Msuva kwa gharama yoyote ile.
“Unajua Msuva tulishazungumza naye muda mrefu na mashabiki wetu wamekuwa wakisukuma sana tumchukue, wanampenda sana kijana wao, kikubwa zaidi ya hapo hata makocha wetu wa sasa ambao hawajawahi kufanya kazi na Msuva, nao wanamtaka sana,” alisema bosi mmoja mkubwa ndani ya Yanga ambaye anagombea nafasi za juu katika uongozi.
Mapema kocha Nabi alisema anatambua Msuva bado yuko katika mgogoro na Waydad, lakini anajua Yanga kama mabosi wake wa GSM watamaliza.
“Nahitaji mshambuliaji mwenye kujua kufunga na kasi, nipo hapa Tanzania kuna wakati ni jambo zuri kuendeleza wachezaji wa taifa hili, natamani sana kufanya kazi na yule Msuva (Simon),” alisema Nabi ambaye ana uraia wa Tunisia na Ubelgiji.