Home Habari za michezo WAKATI CHUPA YA MVINYO WA SIMBA KUHUSU MABADILIKO IKIWA INACHAKAA…CHUPA YA YANGA...

WAKATI CHUPA YA MVINYO WA SIMBA KUHUSU MABADILIKO IKIWA INACHAKAA…CHUPA YA YANGA NDIO KWANZA MPYAAA…


Na  Mohammed Kuyunga/MwanaSpoti

KUNA watu wana maneno ya shombo. Unakumbuka kuna mheshimiwa mmoja aliwahi kuwambia wenzake wanafikiria kupitia makalio?

Bado, kuna mwengine aliwahi kuwaamwambia mwenzake amekula maharage ya wapi?

Kuna ndugu yangu mwingine aliwahi kusema ‘wale jamaa sijui wanatumia sigara gani pale?’

Haya yote yanatokana na ulevi fulani hivi. Kuna mtu hawaelewi wenzake wanawaza nini hadi kufikia hatua ya kumuona yeye hayuko sawa.

Ndio kilevi. Leo hii Yanga huwezi kuwaambia kitu kihusu kilevi chao Injinia Hersi na Kampuni ya GSM. Kilevi chao ndio kwanza kinafunguliwa kizibo kwenye chupa. Mtu yeyote wa Yanga kwasasa huwezi kumtenganisha na Hersi pamoja na wadhamini wao hao.

Hawana baya Jangwani

Wadhamini hao na Hersi hawana baya kwa Yanga. Huwezi kuwaambia kitu kwa sababu wakikumbuka katika miaka minne walikuwa wakiishi kwa kupata furaha robo na maudhi nusu na robo.

Nani amesahau Yanga ilivyotembeza bakuli wakati watani wao wa jadi, Simba Sports wakiwa kwenye neema chini ya uwekezaji wa Mohammed Dewji ‘MO’?

Umesahau kauli ya Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kwenye Tamasha la Kubwa Kuliko?

Rais Kikwete alikiri hali ilikuwa mbaya sana ndani ya klabu hiyo, huku wakilazimika kupigiana simu kujua timu inawezaje kusafiri kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

Mkumbuke Haji Manara

Hali hii sio kama haijawahi kutokea Simba. Unaikumbuka kauli ya Haji Sunday Manara alipokuwa Msimbazi baada ya ujio wa MO?

Manara alisema watu wengi walikuwa hawajui tu, kabla ya ujio wa tajiri huyo, Simba ilikuwa na hali mbaya sana na walikuwa wakijitahidi kutafuta watu wa kuisadia kwenye safari zake za kucheza Ligi Kuu.

Ujio wa MO uliwafanya mashabiki na wanachama wa Simba kutamba na kuamini walikuwa na haki ya kushinda kila mechi na kila taji waliloshiriki.

Kumbuka kauli ya Kwa Mkapa hatoki mtu. Aly Ahly, JS Saoura, AS Vita na wengine walikuja kuchezea vichapo jijini Dar es Salaam.

Kiburi kiliwafanya wengine kukufuru wakisema ‘aliyemleta Chama peponi moja kwa moja’.

Kipindi hiki cha miaka minne ilikuwa ni vigumu mno kumwambia shabiki au mwanachama wa Simba kuwa MO hafai.

Hata kuhusu ile Sh20 bilioni ambayo tajiri huyo alitakiwa aiweke, wengine walisema kabisa aiweke asiiweke wao wanachotaka ni furaha tu ambayo ilikuwa ikipatikana.

SOMA NA HII  DEAL DONE....MKANDARA AKAMILISHA SAFARI YAKE YA KUTUA AZAM FC....SASA MAMBO NI 'BULIBULI'....

Kina Hamisi wawili na MO

Wa kwanza kuupinga uwekezaji wa MO alikuwa ni Mzee Hamisi Kilomoni. Huyu ameshawahi kuwa mchezaji wa Simba, kiongozi na mdhamini wa klabu hiyo.

Hata hivyo, wanachama na mashabiki wa Simba hawakumwelewa. Wengi walisema wazee hao wamepitwa na wakati.

Mtu wa pili alikuwa Dk. Hamisi Kigwangwala (mb). Lakini na yeye chamoto alikiona.

Alishambuliwa kwa maneno na mashabiki na wanachama wa Simba kila kona. Ni kwasababu kilevi kwenye chupa ya mashabiki hao kilikuwa bado hakijaisha.

Hakuna shabiki wala mwanachama wa Simba aliyethubutu kuungana hadharani na kina Hamisi hao wawili.

Kilevi kimekwisha Msimbazi

Leo kilevi kimekwisha, wanaibuka wengine kuikosoa Simba na MO, kuhusu mchakato wa ubinafsishaji wa klabu yao. Wanasema hivyo kwa sababu kilevi chao kimekwisha baada ya miaka minne.

Mwenyekiti wa zamani wa Simba, Ismail Aden Rage, huyu ni mwanachama mkubwa sana ndani ya Simba, leo naye anajitokeza hadharani kuungana na Kigwangwala na Mzee Kilomoni!

Alikwina (alikuwa wapi?), Mwina Kaduguda naye anakuja na mtazamo mwingine kuhusu uwekezaji naye alikuwa wapi.

Huyu ameshawahi kukaimu nafasi ya mwenyekiti wa Simba, baada ya Sweddy Mkwabi kujiuzulu.

Bahati mbaya zaidi, mpaka leo Mkwabi amefunga mdomo wake hajasema kile alichokiona ndani ya Simba.

Kufungua na kufunga vikao

Rage anasema Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu kazi yake ni kufungua na kufunga vikao tu, hana shughuli nyingine. Kwani Rage hakushiriki mchakato na kutoa mawazo yake kuhusu hadhi ya mwenyekiti wa Simba kwenye mabadiliko?

Kwa nini leo? Au kwa sababu kilevi cha furaha ya ubingwa wa miaka minne kimekwisha?

Leo hii utawaambia nini Yanga, kuhusu Injinia Hersi Saidi kuwania nafasi ya Urais ndani ya Yanga.

Yanga imefanya mabadiliko ya katiba kuhusu kupiga kura kwenye Mkutano Mkuu kwa sasa wanachama watano watapiga kura kwa niaba ya kila tawi kuchagua viongozi. Hakuna anayejali kwa sasa kwa kuwa kilevi kitamu ndio kwanza kimeanza kuwalewesha.

Injinia Hersi anaingia Yanga kwa miguu miwili, anakwenda kulinda mali za Yanga na maslahi ya GSM. Ni kama MO alivyomteua, Barba Gonzalez kuwa mtendaji mkuu wa klabu ya Simba.

Huyu bundi anahama, Simba na Yanga. Mwenyekiti wa Yanga, Mshindo Msola aliikaribisha GSM na Injinia Hersi ndani ya klabu hiyo, kwa sasa hatoshi tena.