Home Habari za michezo BAADA YA KUONA ‘CHAMA’ LAO HATARINI KUPOTEA LIGI KUU…MABOSI MTIBWA SUGAR WAIBUKA...

BAADA YA KUONA ‘CHAMA’ LAO HATARINI KUPOTEA LIGI KUU…MABOSI MTIBWA SUGAR WAIBUKA NA HILI JIPYA….


Uongozi wa Mtibwa Sugar umeweka mpango mkakati wa kuhakikisha kikosi chao kinashinda michezo yote ya Ligi Kuu iliyosalia msimu huu 2021/22, wakianza na mchezo dhidi ya Ruvu Shooting utakaopigwa Jumatatu (Juni 13) katika Uwanja wa Manungu Complex mkoani Morogoro.

Mtibwa Sugar imekua na matokeo ya kutoridhisha msimu huu, hali ambayo imeiweka timu hiyo kwenye orodha ya timu zinazopambana kukwepa kushuka daraja.

Afisa mtendaji Mkuu wa Mtibwa Sugar Saad Kawemba amesema, bado wana nafasi kubwa ya kuhakikisha timu yao inabaki Ligi Kuu kwa msimu ujao, hivyo wamejipanga kuhakikisha wanashinda michezo yote iliyosalia.

Amesema Mtibwa Sugar itacheza michezo miwili nyumbani na mingine wiwili ugenini, na tayari Benchi la Ufundi chini ya Kocha Salum Mayanga limejizatiti kuchuma alama zote 12 za michezo hiyo.

“Tuna michezo miwili nyumbani na mingine miwili ugenini, kwenye karatasi inaonekana ni michezo yenye changamoto kubwa ya ushindani, lakini sisi tunaamini kwamba bado tunaweza kupata matokeo kwenye michezo hiyo,”

“Tunaamini tukipata alama 12 ama alama 09, tutakuwa kwenye eneo sahihi katika msimamo wa Ligi, kwa sababu hakutakua na timu yoyote ambayo itaweza kutufikia.” Amesema Saad Kawemba

Naye Kocha Misaidzi wa timu hiyo Awadh Juma amesema: “Jumatatu tutakua na mchezo mgumu sana kwetu, na hata kwa wenzetu, tunahitaji matokeo kwenye mchezo huo, tumewaandaa wachezaji wetu katika hali ya kwenda kushindana, na tumeridhishwa na maendeleo yao.”

“Benchi la Ufundi tunaamini wachezaji wetu watakwenda kupambana dhidi ya Ruvu Shooting ili tuanze kufanikisha mpango wetu wa kubaki Ligi Kuu tukiwa nyumbani Manungu Complex, tumejipanga kuhakikisha tunaukamata vizuri mchezo huo ndani ya dakika 90 na hatimaye tuweze kupata alama tatu muhimu.”

Mtibwa Sugar iliyoshuka Dimbani mara 26 hadi sasa, imejikusanyia alama 28 zinazoiweka kwenye nafasi ya 12 katika msimamo wa Ligi Kuu, huku Mpinzani wake mtarajia Ruvu Shooting akiwa nafasi ya 13 baada ya kucheza michezo 26 na kukusanya alama 28.

SOMA NA HII  WABABE WA YANGA WAANZA TAMBO...KUMBE WALIMFANYIA MAZOEZI SPESHO AZIZ KI