Home Habari za michezo KUELEKEA MSIMU UJAO…MABOSI SIMBA WAAZIMI KUTIKISA AFRIKA KWA USAJILI…’MASHINE’ HIZI ZA KAZI...

KUELEKEA MSIMU UJAO…MABOSI SIMBA WAAZIMI KUTIKISA AFRIKA KWA USAJILI…’MASHINE’ HIZI ZA KAZI KUTUA ….


MABOSI wa Simba wameitana ghafla jijini Dar es Salaam na kufanya kikao kizito ikiwa ni saa chache tangu wamfurushe aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Pablo Franco na kuazimia kushusha mashine kali za kutengeneza kikosi cha kibabe kwa msimu ujao.

Kikao hicho kinachoelezwa kiliwahusisha baadhi ya Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba pamoja na Mtendaji Mkuu, Barbara Gonzalez iliamua kwa pamoja kusajili nyota wapya wanne wa kimataifa kuchukua nafasi ya itakayowatema waliopo kikosini kwa sasa, miongoni mwao ni Mcameroon aliye mkali wa mabao na wa Afrika ya Kati mwenye asili ya DR Congo.

Wanene hao wa Msimbazi, wamekubaliana kuleta mashine hizo ili kuimarisha maeneo yao manne wanayoamini msimu huu yamewaangusha na kila idara wameweka machaguo manne ili mmoja akizingua basi iwe rahisi kwao kumbeba yeyote na kuimarisha kikosi chao kwa msimu ujao.

Gazeti la Mwanaspoti limepenyezewa na kuchapisha dondoo za kikao hicho na kuelezwa, Simba inataka kuleta beki mpya wa kati, kiungo mkabaji, kiungo mshambuliaji pamoja na straika wa maana ili atupie sana nyavuni baada ya msimu huu eneo hilo kushindwa kufanya makubwa tofauti na msimu uliopita.

Katika orodha hiyo, katika eneo la ushambuliaji mabosi hao wa Simba wana majina matatu waliovutiwa nao na mmoja kati yao anatarajiwa kuvaa uzi wa timu hiyo kwa msimu ujao, huenda mmoja kati ya huyo atakuja kuvaa jezi ya Simba msimu ujao.

Chaguo la kwanza na pili limeenda kwa Mzambia Moses Phiri ambaye inaelezwa kila kitu chake kwa ajili ya kutua Msimbazi kimekamilika kwa sasa akitokea Zanaco, huku chaguo la tatu likiwa ni straika Mcameroon, Frank Mbella Etouga anayekipiga Asante Kotoko ya Ghana alijiunga mwaka jana ambaye rekodi zake zinaonyesha katika mechi 19 amefunga mabao 15.

Etouga mwenye umri wa miaka 20 anakipiga pia timu ya taifa ya Cameroon na kabla ya kutua Asante Kotoko alipita AS Fortune de Mfou alikoichezea mechi 21 na kufunga mabao nane, huku akipita pia Nkufo Academy alikoichezea mechi 30 na kuweka kambani jumla ya mabao 61.

SOMA NA HII  YANGA KAZI INAENDELEA KWA AJILI YA MSIMU MPYA WA 2021/22

Jina jingine la mwisho kwenye eneo hilo ni la kinra wa mabao wa Ligi Kuu ya Uganda, Cesar Lobi Manzoki Mkongoman aliyechukua uraia wa Afrika ya Kati, katika maeneo mengine yana wachezaji kutoka Afrika Kusini, Nigeria na Zambia ambao watachukua nafasi ya watakaotemwa.

“Kikao kimepitia majina yote wa kila kwenye eneo, ila mjadala ulikuwa kwa mastraika, kwani licha ya uhakika wa Moses Phiri, lakini alihitajika mkali mwingine hasa huyu Mcameroon, hata hivyo maamuzi ya mwisho yatatolewa baada ya kumalizika kwa mechi za Ligi Kuu,” kilisema chanzo chetu, huku majina ya Bernard Morrison aliyeondolewa kikosini, Pascal Wawa, Meddie Kagere, Taddeo Lwanga yakiwa ni kati ya watakaozibiwa nafasi zao.

Pia inaelezwa kuna mvutano mkubwa juu ya maamuzi ya kuwapiga chini au kuwabakisha ya Peter Banda na Chris Mugalu.