Home Habari za michezo PAMOJA NA KUCHECHEMEA MSIMU HUU…REKODI YA KAGERE BADO YADAI LIGI KUU…SI MPOLE...

PAMOJA NA KUCHECHEMEA MSIMU HUU…REKODI YA KAGERE BADO YADAI LIGI KUU…SI MPOLE WALA MAYELE ANAYEIWEZA…


Mastraika wanaoongoza kwa mabao 14 Ligi Kuu Bara, Fiston Mayele wa Yanga na George Mpole wa Geita Gold wana kazi ngumu kuifikia rekodi ya Meddie Kagere.

Katika msimu wa 2018/19 Kagere wa Simba alifunga mabao 23, huku uliofuata wa 2019 -20 akifunga mabao 22 aliyoshindwa kuyafikia msimu ulioisha alipomaliza na mabao 14 ambayo ndio wanayomiliki Mayele na Mpole kwa sasa. Kutokana na kiwango kinachoonyeshwa na Mayele na Mpole msimu huu katika mechi nne zilizosalia wanaweza kuzalisha mabao tisa ili kufikia idadi ya mabao 23 ya Kagere aliyofunga kwa misimu miwili mfululizo?

Kutokana na mwenendo wa ufungaji wa washambuliaji hao staa wa zamani wa Yanga, Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ ambaye ana rekodi tamu zaidi ya ufungaji katika ligi alitoa mtazamo wake dhidi ya mastaa hao wanaotamba kwa sasa.

Mmachinga aliyefunga mabao 26 mwaka 1999, alisema Mayele na Mpole wanatakiwa kuanza kuvunja rekodi ya John Bocco ya mabao 16 ya msimu ulioisha, kisha ya Kegere ya misimu miwili.

“Rekodi ya Bocco inaweza ikawa rahisi kwao, lakini wakikomaa waanze na hiyo ya mabao 22 ya Kagere kabla ya kufikia yangu inayoonekana kuwa ngumu zaidi kwao, maana hadi sasa imeishi kwa miaka 23,” alisema.

Naye straika mwenye rekodi ya mabao 25, mchezaji wa zamani wa Mtibwa Sugar, Abdallah Juma alisema haoni anayeweza kufikia mabao 22 ya Kagere msimu huu.

“Mechi zilizosalia ni chache kuliko walizocheza. Ndio maana sioni uwezekano wao kumaliza na mabao 22, labda wataanza na hiyo ya mabao 16 ya Bocco aliyofunga msimu ulioisha na changamoto wanakutana na timu zinazojikwamua kutoshuka daraja,” alisema.

Hata hivyo, Mpole akizungumzia hilo alisema anatanguliza maslahi ya timu kuliko binafsi, ingawa zikitokea nafasi za kufunga atafanya kweli. “Unaweza kumaliza na mabao mengi lakini timu ikiwa chini hilo halisaidii, maana yangu ikitokea nina nafasi ya kufunga nitafunga kama ni kutoa asisti nitafanya,” alisema.

Kagere tangu ajiunge na Simba 2018-2022 amefunga mabao 66 Ligi Kuu Bara.

SOMA NA HII  SOKA LINAENDELEA NDANI YA DStv....BAADA YA KUMALIZANA NA WANAUME..SASA UELEKEO NI HUU...MSELELEKO NI ULE ULE...