Home Geita Gold FC RUNGU LA FIFA LAWAFANYA GEITA GOLD KUITANA KUMJADILI NDAYIRAGIJE..WADAI KUNA VIFUNGU VYA...

RUNGU LA FIFA LAWAFANYA GEITA GOLD KUITANA KUMJADILI NDAYIRAGIJE..WADAI KUNA VIFUNGU VYA KIMKATABA…


Mabosi wa Geita Gold wamekiri kupokea taarifa ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) juu ya kufungiwa kusajili wachezaji kwa kosa na kushindwa kumlipa aliyekuwa kocha yao, Etienne Ndayiragije na kusema watakaa pamoja kujadiliana kwa kina.

TFF ilitoa taarifa juzi jioni, Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA), limeifungia klabu hiyo kusajili kwa kushindwa kumlipa fidia ya kuvunjiwa mkataba na malipo yake mengine na kama itashindwa kutekeleza hilo, itafikishwa Kamati ya Nidhamu ya FIFA kwa adhabu zaidi.

Ofisa Habari wa Geita, Hemed Kivuyo alisema uongozi wao utakutana leo Jumatatu ili kujadili jambo hilo na mambo mengine ya klabu hiyo.

“Taarifa imetoka alasiri Ijumaa na juzi na jana ni wikiendi, halafu uongozi ni wa Halmashauri, hivyo sio rahisi kukaa kikao cha haraka,” alisema Kivuyo.

Kivuyo alikiri kocha huyo kudai lakini kwenye mkataba kuna vifungu vya makubaliano kwa hiyo watatoa taarifa rasmi.

“Kimsingi anachodai ni fidia kama taarifa inavyosema lakini mikataba huwa ina vifungu kadhaa vya makubaliano, uongozi ukikaa na kamati na kunipa taarifa rasmi nitawajuza mapema,” alisema Kivuyo.

Rungu la FIFA limeangukia pia upande wa Biashara United kufungiwa madirisha mawili ya usajili baada ya kushindwa kuheshimu uamuzi wa awali wa FIFA kumlipa mshahara mchezaji wao Timoth Omwenga.

Ofisa Habari wa Biashara, Salma Thabit na alikiri kuona taarifa hiyo lakini alisema hawezi kuzungumzia kwa sasa.

“Uongozi wote wameona taarifa hiyo lakini hakuna wa kuzungumzia kwa sasa, tunafikiria hii mechi yetu ya leo (jana) na namna tutakavyomaliza Ligi,” alisema Salma.

SOMA NA HII  AL AHALY, WYDAD NA SIMBA ZATAJWA CHANZO CHA CAF KUTAKA KUFUTA KOMBE LA SHIRIKISHO..