Home Habari za michezo TAMBWE: SICHEZI TENA LIGI YA DARAJA LA KWANZA….UMIMI UMEIPONZA DTB…..KILA MCHEZAJI ANAJIONA...

TAMBWE: SICHEZI TENA LIGI YA DARAJA LA KWANZA….UMIMI UMEIPONZA DTB…..KILA MCHEZAJI ANAJIONA BORA…


KUNA mtu amefanya kazi kubwa kwenye Simba na Yanga. Anaitwa Amissi Tambwe. Ndani ya miezi yake 18 kwenye klabu ya Simba, Tambwe alifunga mabao 20 ya Ligi Kuu.

Straika huyo alifunga mabao 19 msimu wa 2013/14 na kuibuka mfungaji bora kabla ya msimu uliofuata kufunga bao moja pekee katika mechi saba za mwanzo wa msimu, jambo lililosababisha kuachwa na Simba ambayo iliamini amekwisha na ikamsajili Danny Sserunkuma kutoka Gor Mahia ya Kenya.

Tambwe akaibukia Yanga ambako alifunga mabao 13 katika msimu wake wa kwanza kabla ya kufunga mabao 21 msimu uliofuata na kuwa mfungaji bora tena. Staa huyo amefanya mahojiano maalum na Mwanaspoti Jijini Dar es Salaam na kufunguka mambo kadhaa ikiwemo sifa za Fiston Mayele;

MAYELE NOMA

“Hakuna shabiki ambaye anaweza kukuelewa ukimwambia Mayele sio mchezaji mzuri. Kwa upande wangu mimi pia ukiniambia nitaje mchezaji mzuri msimu huu ndani ya Yanga siwezi kusita kutaja hilo jina,” anasema.

Tambwe mbali na kukiri ubora wa Mkongo huyo pia amefunguka kuwa kwa aliyoyafanya yeye ndani ya Simba na Yanga kuna washambuliaji hawajayafikia hivyo pia anatakiwa kupewa heshima yake na siyo kusahaulika kirahisi.

Mcheza huyo wa Singida Big Stars iliyopanda Ligi Kuu Bara kucheza msimu wa 2022/23 anasema Championship ni kugumu sana.

Akiapa hata akipewa mamilioni kiasi gani, hawezi kukubali kucheza ngazi hiyo endapo kama Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) halitaboresha baadhi ya mambo.

Anasema Ligi ya Championship ni ngumu kutokana kutokuwepo kwa wadhamini huku akizikosoa mamlaka kutomulika kwa ukaribu suala la nidhamu mbovu kama wachezaji kuumizana kwa makusudi.

“Tofauti na Ligi Kuu ambako mechi zinafuatiliwa na vyombo vya habari, inakuwa ngumu mchezaji kufanya rafu ama vitendo vya utovu wa nidhamu, wakijua watashitakiwa na TFF,” anasema.

“Na huko Championship kuangaziwe ili wachezaji wawe na amani kuonyesha vipaji vyao, tofauti na niliyoyaona, nimechezewa rafu hadi sitamani kucheza tena huko chini.

Anasema: “Daraja la Kwanza wachezaji wanapigana uwanjani na hata mwamuzi pia asipokaa sawa anaweza kupigwa, hii ni kutokana na ligi kutoonyeshwa tofauti na ilivyo kwa upande wa Ligi Kuu, huku chini kuna changamoto kubwa sana na ni kugumu.”

TIMU ZA JESHI

Tambwe ana historia na timu za jeshi kutokana na namna ambavyo aliwahi kuchezewa rafu tangu yupo Simba, Yanga na Singida.

“Uso wangu una mishono isiyohesabika, kutokana na kuchezewa rafu hasa dhidi ya timu za jeshi, yaani hadi sasa nikiwa DTB(Singida Big Stars) pia nimeshonwa mara nyingi baada ya kuchezewa rafu,” anasema Tambwe na kuongeza;

“Kuna wakati nikikutana na aliyenichezea rafu wakati nipo Yanga akanikaba hadi nikatokwa na damu, nikimuona mwili unasisimka na moyo unashituka, maana niliepuka kifo, yaani maumivu niliyoyapata sitayasahau kabisa.

AZIGOMEA TIMU ZA LIGI KUU

Anasema wakati wa usajili wa dirisha dogo, alitafutwa na timu tano za Ligi Kuu Bara ambazo ni KMC, Tanzania Prisons, Geita, Mtibwa Sugar, Kagera Sugar na Coastal Union zikionyesha nia ya kumsajili. “Sikutaka kuachana na DTB kipindi hicho kwasababu ndoto yangu ilikuwa ni kuhakikisha naipandisha timu Ligi Kuu nashukuru Mungu nimefanikisha hilo japo haikuwa rahisi,” anasema.

ALIVYOMPATA MKEWE

Safari ya kumpata mke wake (Raiyan) maarufu kwa jina la Ray wa Tambwe, ina fundisho ndani yake kwa vijana wanaosaka wenza.

Tambwe anasema anakumbuka Yanga ilicheza dhidi ya Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine, akafunga bao lililomchukiza mrembo huyo kiasi cha kumuona ana sifa.

“Alikuwa ananichukia kuna watu walimsikia akisema Tambwe anataka sifa sana kwani kulikuwa na ulazima gani wa kuifunga Mbeya City, maana yeye alikuwa ni shabiki wa Simba, nikaambiwa, ikabidi nimtafute na kumwambia soka ni amani na kazi yangu ni kufunga,” anasema na kuongeza;

“Tukabadilishana namba tukaanza kuwasiliana hadi ikafikia hatua ya kufunga ndoa, kinachonishangaza ni namna alivyobadilisha mapenzi yake kuipenda Yanga wala bila kulazimisha na nampelekea jezi ya Wananchi.”

UKOCHA MH! PRESHA

“Sijajua ni lini nitastaafu soka, ila muda ukifika nitatoa taarifa lakini kwasasa bado ni mchezaji na nitaendelea kuwepo kwenye Ligi Kuu msimu ujao baada ya kuipandisha DTB,” anasema na kuongeza:

“Hata ikitokea nikaamua kustaafu siwezi kusomea ukocha sio ndoto yangu na siwezi kwasababu kufundisha mpira inahitaji moyo sana siwezi maana naweza kufa kwa presha.”

SOMA NA HII  USAJILI WA MASTAA WAPYA YANGA WATINGA CAF...MAMBO YOTE YAANIKWA HADHARANI...JINA LA MORRISON KAMA KAWA....

Anasema akicheza soka amekuwa akishuhudia makocha wengi ambao wanafundisha namna wanavyopata tabu hasa timu inapopata matokeo mabaya tofauti na vile walivyotarajia hivyo anaamini kwa upande wake kazi hiyo haiwezi na mipango yake ni kufanya biashara.

SABABU YA DTB KUKOSA TAJI

DTB imepanda daraja itacheza Ligi Kuu msimu wa 2022/23 lakini ilishindwa kutwaa taji la ligi hii pamoja na kuongoza kwa muda mrefu. Staa na kinara wa timu hiyo amefunguka kilicho waangusha.

“DTB tumeongoza ligi kwa muda mrefu lakini mechi za mwisho tuliridhika na kujiona tayari tumeshamaliza na naamini kilichotuponza ni kutokana na timu kuwa na wachezaji wengi wazoefu hivyo kila mmoja alikuwa anajikuta staa wa timu,” alisema na kuongeza;

“Umimi umetuponza. Kila mchezaji alikuwa anajiona yeye ni bora kuliko mwingine na ilifika wakati tulishindwa kufanya kazi kwa kushirikiana,” anasema.

KILICHOMKIMBIZA DJIBOUTI

Anasema kabla hajarejea Tanzania kuungana na DTB alikuwa Djibouti ambako alikuwa anacheza timu inayoshiriki Ligi kuu nchini humo lakini alishindwa kubaki huko pamoja na kupewa ofa ya kuongeza mkataba kutokana na hali ngumu ya maisha.

“Nilicheza msimu mmoja na nilikuwa namba mbili kwenye washambuliaji waliofunga mabao mengi lakini maisha ya nchini humo ni magumu sikuweza kuvumilia kuanzia vyakula, hari ya hewa kule jua ni kali sana yaani Dar es Salaam cha mtoto, kule kuna bahari nyekundu, umewahi kuiona?

“Kitu ambacho kilikuwa kinanishangaza zaidi kule ng’ombe wanakufa tu barabarani kutokana na hali ya hewa, jua ni kali sana linaunguza balaa pia nilishashuhudia kunguru wakidondoka kutokana na hali hiyo ya jua kali,” anasema na kuongeza:

“Nilikuwa na ofa nyingi na timu za Ligi Kuu sio madaraja ya chini lakini huwezi kuamini nilishindwa kubaki Djibouti, niliamua kurudi Tanzania na kuja kucheza Daraja la Kwanza hii ni kutokana na kupata fedha kubwa pamoja na kuzoea mazingira ya hapa.

“Mimi bado ni mchezaji wa DTB, nina mkataba nao lakini kama kuna timu inanihitaji inatakiwa kufanya mazungumzo na uongozi wa timu yangu naweza kucheza popote bila kujali, ninachokiangalia sasa ni maslahi.

“Nina uwezo wa kucheza timu yoyote ya Ligi Kuu nina uzoefu wa kutosha pia nina rekodi zangu siwezi kuhofia chochote najiamini na nina uwezo wa kucheza.”

ANA KIWANJA MBEZI

“Naipenda Tanzania ni nchi iliyobarikiwa amani na ina wananchi waungwana wasio na mambo mengi kama kufuatilia maisha ya mtu binafsi, sifa hizo zimenifanya nishawishike kuwa na mji hapa nina kiwanja Mbezi nilikinunua kabla sijaondoka Yanga,” anasema na kuongeza kuwa:

“Namiliki kiwanja tu kwasasa sijafahamu ni lini nitakijenga lakini hadi nimekinunua maana yake nia ni kuwa na makazi hapa pia, Mungu akijaalia uzima ntalikamilisha hilo. Mbali na hapo sina kitu kingine ninachomiliki.”

FAMILIA ITABAKI BURUNDI

Tambwe ambaye ameoa Tanzania amethibitisha kuwa pamoja na kurudi hapa na kupata timu inayocheza Ligi Kuu hana mpango wa kuirudisha tena familia yake huku kutokana na watoto wake kuwaanzisha shule Burundi.

“Ni kweli tangu nimeanza kucheza Simba na baadaye Yanga nilikuwa na familia yangu hapa, lakini nilipoondoka nchini nilihama nayo na sasa sina mpango wa kuirudisha tena kwasasabu wanangu wawili wameshaanza shule sitaki kuwahamisha na kama watakuwa wamenikumbuka hapa sio mbali watakuwa wanakuja kunisalimia.”

KIKOSI CHAKE

Kipa ni Beno Kakolanya, Juma Abdul, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Kelvin Yondani, Vincent Bossou, Jonas Mkude, Mbuyu Twite, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Donald Ngoma na Amissi Tambwe. Katika kikosi hicho Tambwe anamtaja Yondani angependa awe nahodha na kocha ni Hans Pluijm.

“Yondani ni beki fundi, kiongozi dhidi ya wengine na kocha Pluijm anafundisha na kumjenga mchezaji kiakili kuhakikisha anafanikisha ndoto zake,” anasema.

KUSHANGILIA SIO ISHU

Anasema amefunga sana na ni mchezaji ambaye amezaliwa kwa kazi hiyo hivyo haoni sababu ya kubuni mbinu ya kushangilia akipata nafasi ya kufunga kama ilivyo kwa Fiston Mayele ambaye amekuwa akitetema.

“Nimefunga sana hakuna asiyemfahamu Tambwe kwenye soka la Tanzania hii ni kutokana na sifa yangu ya kutupia nyavuni mara kwa mara hivyo sina sababu ya kubuni namna ya kushangilia nikifunga zaidi ya kupeleka mpira kati na kuendelea kucheza,” anasema na kuongeza kuwa hana hofu na Ligi Kuu ambayo ameizoea na ametamba ataendelea kutupia sana tu.