Baada ya kukaa nje ya Uwanja kwa nusu msimu, mshambuliaji Yacouba Sogne, huenda akajiunga na Geita Gold FC kwa ajili ya msimu ujao.
Yacouba ameshindwa kutamba msimu huu kutokana na kusumbuliwa na majeraha anatajwa kutua timu hiyo ambayo inatarajia kuiwakilisha nchi kwenye mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika mapema Agosti mwaka huu.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Yanga kimethibitisha kuwa staa huyo hatakuwa miongoni mwa wachezaji watakaoiwakilisha Yanga msimu ujao wa Ligi Kuu Bara, Ligi ya Mabingwa Afrika na mashindano mengine kwani mkataba wake umemalizika na hajaongezwa.
“Geita wamekuja kutuomba mchezaji huyo ili aweze kuwasaidia msimu ujao na kwenye mashindano ya kimataifa hatukuona sababu ya kuendelea kumkatalia wakati hayupo kwenye mipango ya kocha,” alisema na kuongeza;
“Yacouba tulikuwa na mpango wa kumuongeza mkataba na kumtoa kwa mkopo ili aweze kwenda kurudisha ubora wake baada ya kukaa nje ya uwanja kwa muda mrefu baada ya kupata ofa ya Geita Gold tumemruhusu afanye mazungumzo na timu hiyo.”
Alipotafutwa Mwenyekiti wa Geita Gold, Leonard Bugomola ambaye alikana kuzungumzia usajili huo akisisitiza kuwa wataweka wazi usajili wao kuanzia Jumatano baada ya kukutana kama kamati ili kuboresha kikosi chao.
“Tulikuwa na mkutano jana ‘Jumanne’ kwaajili ya kujadili usajili utakaoweza kutubeba kwenye mashindano ya ndani na kimataifa na ni msimu wetu wa kwanza kushiriki,” alisema na kuongeza;
“Tunahitaji wachezaji wenye uzoefu na uwezo mkubwa utakaokuwa chachu ya mafanikio kwenye msimu wetu wa kwanza tunahitaji kujifunza kutoka kwa waliotutangulia hivyo tunahitaji kuwa bora na kufanya vizuri.”
Hadi sasa, Geita imemsajili Ramadhan Chombo ‘Redondo’ aliyethibitisha kusaini mkataba wa miaka miwili.