Kocha Zoran Maki juzi aliishuhudia timu yake kwa mara ya kwanza ikicheza mechi ya kirafiki dhidi ya Ismaily ikiwa kambini Ismailia, Misri na kuvutiwa na soka tamu lililopigwa na vijana wake, huku akipagawa zaidi baada ya wachezaji watano akiwamo Moses Phiri na Henock Inonga kutua.
Nyota hao watano walichelewa kuondoka kwenda kambini kutokana na ishu ya viza, hivyo kuwashuhudia wenzao 19 wakitangulia Alhamisi iliyopita.
Sasa kutua kwa wachezaji hao na namna Zoran alivyokiona kikosi hadi sasa hasa kupitia mchezo wao wa kwanza wa kirafiki dhidi ya Ismaily ulioisha kwa sare ya 1-1, bao la Simba likiwekwa kimiani na kiungo mpya, Augustine Okrah, kumemfanya kocha Zoran kupagawa na kufunguka alivyofurahi.
Zoran alisema amefurahia namna timu ilivyocheza japo amekaa nao kwa muda mfupi na kwamba amepata moja ya vipimo anavyohitaji kuona jinsi mazoezi waliyofanya yalivyopokewa na kufahamu viwango na uelewa uliopo wa kushika mambo.
Alisema amefurahishwa kukutana wa wachezaji wenye viwango bora na uharaka wa kuelewa aina ya mazoezi na mbinu anazowapatia tena ndani ya muda mfupi ingawa bado kuna maeneo yana changamoto na atayaweka vizuri.
Kuhusu Okrah, alisema ni mmoja ya wachezaji ambao ndani ya muda mfupi wameonyesha ubora walionao kutokana na kile alichowaelekeza na anaamini akikaa nao kwa muda mrefu watakuwa bora zaidi na kuibeba timu hiyo.
“Kama nilivyowaona wachezaji wengine wapo kwenye viwango bora, Okrah ni miongoni mwao, amefanya vizuri na amecheza kama timu ilivyokuwa ikihitaji kutoka kwake,” alisema Zoran na kuongeza;
“Kuhusu wachezaji wapya hadi sasa waliopo kambini wameonyesha walistahili kusajiliwa kwani wamecheza mechi hiyo na wamefanya mazoezi vizuri bila shida yoyote kama wapo kwenye timu kwa muda mrefu.”
Kwa wachezaji waliomaliza msimu, alisema wamemsaidia kumpa ramani ya maisha ndani ya klabu na kwamba wanaishi vizuri na wale wapya huku wakifanya kazi kwa pamoja na ushirikiano mkubwa na kusema hiyo ndio maana halisi ya timu.
“Tunaendelea na ratiba ya mazoezi ya awamu mbili kwa siku. Kuna nyakati tutafanya yale magumu zaidi ya Gym ili kuendelea kuweka miili yao kwenye hali ya ushindani.”
Zoran alisema ratiba ya mechi za kirafiki watacheza nne au tano baada ya Ismaily na kusisitiza anataka mechi ngumu zaidi ili kupima uwezo wa wachezaji kabla ya kurejea nchini mwanzoni mwa Agosti.