Kiungo mshambuliaji, Bernald Morrison kurejea tena Yanga si jambo la ajabu, lakini ana kazi kubwa ya kufanya mashabiki wake waendelee kumheshimu.
Kwa mara ya kwanza Morrison ambaye ni raia wa Ghana kuichezea Yanga ilikuwa 2020 kwa muda wa miezi sita, kisha akajiunga na Simba 2020 hadi 2022 na Ligi Kuu msimu ujao wa (2022/23) atavaa uzi wa kijani.
Haya hapa mambo matano ambayo Morrison akiyafanya kwa usahihi, heshima ya kiwango chake itaendelea kuwa imara na kupendwa na mashabiki wake.
Nidhamu
Kitendo cha Morrison kuhamia Simba kulikoifanya Yanga imshitaki CAS na akashinda kesi, awamu hii atakuwa na kazi kubwa ya kuonyesha nidhamu ndani na nje ya uwanja kuhakikisha inawavutia mashabiki wake.
Ukiachana na mashabiki, kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi ni muumini wa nidhamu, jambo litakalomlazimu Morrison kuonyesha mfano dhidi ya nyota aliowakuta ndani ya klabu hiyo.
Kiwango bora
Kitendawili cha kwa nini kamati ya usajili imemrejesha Morrison kwa mara nyingine Yanga? Kitajibiwa na nyota huyo kwa kuonyesha huduma yake muhimu dhidi ya wale aliowakuta ndani ya timu.
Kurejea kwa Morrison Yanga wapo mashabiki waliyofurahia na wengine kuchukizwa na hilo, ili afanikiwe kuwaunganisha wafuasi hao kuwa kitu kimoja ni kuonyesha uwezo mkubwa utakaoinufaisha timu.
Pia ni mtihani kwake kuhakikisha analinda heshima ya kipaji chake alichokionyesha tangu atue nchini.
Rekodi
Katika nafasi anayocheza Morrison alikuwepo Said Ntibazonkiza ‘Saido’, ambaye msimu ulioisha alifunga mabao saba na asisti za kutosha, rekodi ambayo Mghana huyo atatakiwa kuivunja na kuandika ya kwake.
Nje na Saido msimu wa 2020/21, Yacouba Sogne alimaliza na mabao manane, hivyo Morrison ana kazi kubwa ya kuhakikisha anakuwa na rekodi za kuvutia msimu ujao.
Pia, utakuwa ni msimu ambao atatakiwa kupambana kuisaidia timu yake kunyakua ubingwa ili awe na cha kujivunia baada ya utumishi ndani ya klabu hiyo.
Kuendana na mazingira
Kwa asilimia kubwa wachezaji waliocheza na Morrison wengi waliondoka Yanga na kubakia wachache kama Feisal Salum ‘Feitoto’, hilo linamlazimu kwenda kujifunza tabia za nyota waliopo namna walivyokuwa wanafanya kazi kwa kushirikiana hadi kuchukua ubingwa.
Anatua na staili gani
Kwa mara ya kwanza wakati anajiunga na Yanga (2020), Morrison alikuwa akifunga bao alikuwa anashangilia kwa kunyanyua mguu mmoja juu huku akitambaa, je ligi ijayo atakuja na staili gani?
Urejeo wa Morrison Yanga umemuibua mchezaji wa zamani wa timu hiyo, Bakari Malima aliyesema heshima ipo mikononi mwa nyota huyo, kulingana na kile na atakachokionyesha uwanjani.
“Kwanza anatakiwa ajue kwa nini anagombaniwa na Yanga, Simba nje na hapo nidhamu yake ikiwa mbovu hakuna kitu kitawavuta kwake, atatakiwa kujituma kwa bidii ili uwezo wake umbebe mbele ya wadau yaani wawe wanazungumzia huduma yake,” anasema.