Baada ya kutua Singida Big Stars, Mathis Lule amesema atafaidi mengi kwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Hans Van Pluijm kutokana na uzoefu alionao, huku akieleza kuwa ishu ya elimu kwake haina nafasi kimsingi amekubaliana na mabosi kuhusu maslahi yake.
Lule alikuwa Kocha Mkuu wa Mbeya City katika msimu uliopita ambapo tayari amethibitisha kujiunga na SBS kwa mkataba wa miaka miwili akipewa jukumu la kuwa Kocha Msaidizi na timu hiyo ambayo inajiandaa na Ligi Kuu ikiwa ni msimu wao wa kwanza na tayari ipo kambini jijini Arusha.
Pia imeelezwa kuwa kocha huyo ametua na kocha wa makipa, Steven Chigundu (wote kutoka Uganda) na tayari wameungana wenzao kwenye benchi la ufundi kambini ilipo timu hiyo jijini Arusha.
Akizungumza kocha huyo raia wa Uganda amesema licha ya elimu aliyonayo leseni A ya CAF, na ile B ya nchini Ujerumani (ICC) haimfanyi kukataa kufanya kazi chini ya Kocha mwingine.
Amesema anaamini kwa maelewano atakayokuwa nayo na Pluijm wataisaidia SBS kuwa na mafanikio makubwa na kwamba lengo ni kuona timu inakuwa na matokeo mazuri kwenye Ligi Kuu na mashindano mengine msimu ujao.
“Sina tatizo kufanya kazi chini ya Pluijm, ambaye ana uzoefu na ni mkubwa kiumri kwangu hivyo yapo nitakayojifunza, kimsingi nimekubaliana na mabosi kuhusu maslahi yangu, mimi naangalia kazi na hata hivyo malengo yetu ni kupata matokeo mazuri suala la elimu silipi nafasi” amesema Lule.
Kuhusu usajili amesema hadi sasa ni kama wameshakamilisha kwa kiasi kikubwa japokuwa yupo ambaye atafunga rasmi dirisha na kwamba tayari wameanza kambi kujiandaa na msimu mpya.
“Mimi nimefika jana usiku hapa Arusha nimeungana na timu tayari, usajili hadi sasa tuko mwishoni ila kuna mtu atahimisha zoezi letu” amesema Kocha huyo.
Pluijm mwenye UEFA Pro, aliwahi kuzinoa timu kadhaa hapa nchini ikiwa ni Yanga, Azam na Singida United, huku Lule akiifundisha Mbeya City kwa mafanikio.