Mshambuliaji wa Singida Big Stars, Amissi Tambwe amesema amerudi kwenye ligi aliyoizoea na kutamba kwa usajili mkubwa uliofanywa na timu hiyo anaiona nafasi yake ya kutwaa tena kiatu cha dhahabu cha Mfungaji Bora msimu ujao.
Tambwe aliyewahi kutamba kwa misimu sita mfululizo katika ligi hiyo akikipiga Simba na Yanga na kunyakua tuzo ya Mfungaji Bora mara mbili 2013-2014 na 2015-2016, huku akifunga jumla ya mabao 73 kabla ya kutimkia FC Fanja na baadae Polisi Djibouti na kurudia DTB (Singida BS).
Tambwe alisema ametoka ligi kwenye ngumu ya Championship ambayo haitamani kurudi tena na kwamba anataka kutumia nafasi waliyoipata kurudisha jina lake katika Ligi Kuu kwa kuanza na kiatu cha dhahabu pamoja na kuipambania timu hiyo ifikie malengo.
“Nina mengi ya kufanya kuhakikisha naonyesha ushindani nawaheshimu washambuliaji waliopo, naamini na wao wana kitu na wanatamani kiatu hivyo kila mmoja apambane kwa anavyoweza kwa upande wangu lengo ni kiatu na kuipambania timu iwewe na ushindani,” alisema na kuongeza;
“Nina uzoefu mkubwa kwenye ligi hakuna asiye fahamu misimu yote niliyocheza nimeweza kufunga mabao zaidi ya kumi staki kusema nitafunga mangapi msimu huu ila nahitaji kiatu.”
Kuhusu kufanya kazi tena na Hans Pluijm aliyeajiriwa SBS, Tambwe alisema ameipokea kwa furaha uteuzi huo kwani ni kocha ambaye amepita chini yake anafahamu mbinu na mipango yake.
“Nimefanya kazi na Hans ni kocha mzuri anamipango mikubwa ataifikisha mbali SBS nafurahi kupita mikononi mwake tena nina mengi ya kuongeza kwenye maisha yangu ya soka kutoka kwake.”
Tambwe aliongeza kuwa anatarajia ushindani mkubwa kutoka kwa timu pinzani na anaiona ligi kuu msimu ujao ikiongezeka ubora kutokana na uwekezaji mkubwa uliowekwa.
SBS iliyokuwa ikifahamika kama DTB, imepanda daraja msimu huu ikiungana na Ihefu na imefanya usajili wa mshambuliaji mmoja tu mzawa Kelvin Sabato kutoka Mtibwa Sugar atakayeungana na Tambwe sambamba na nyota wengine wa kikosi hicho kilichoanza kambi mapema.