Wakati Kikosi cha Azam FC kikiwa kimeshafika El Gouna-Misri kwa ajili ya Kambi ya Maandalizi ya Msimu mpya wa Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ na Michuano ya Kimataifa (Kombe la Shirikisho Barani Afrika), Kocha Mkuu wa klabu hiyo Abdi Hamid Moallin amefunguka kuhusu Simba SC.
Kikosi cha Azam FC kiliondoka Dar es salaam mapema jana Ijumaa (Julai 22) kuelekea Misri, ambapo kitakua huko hadi mwanzoni mwa mwezi Agosti.
Kabla ya kuondoka Dar es salaam, Kocha Moallin alisema wanakwenda Misri kujiandaa na Kambi ya msimu mpya na wanaamini kwa muda wote watakaokuwa huko watakua na maandalizi mazuri, huku akijikita kwenye mpango wa kutengeneza mfumo mpya wa kupambana dhidi ya timu pinzani.
”Jambo la muhimu tunataka kutengeneza mfumo mpya kwa wachezaji kwa ajili msimu ujao kwa kuwapa mambo ya kiufundi zaidi ili kuwa na kikosi bora na cha ushindani zaidi.” Amesema Kocha Moallin
Amesema wamepanga kucheza michezo ya kirafiki, lakini akasisitiza kutamani kucheza dhidi ya Simba SC ambayo ipo Misri kwa zaidi ya juma moja sasa, ikijiandaa na msimu mpya.
“Tutakua na michezo mingi ya kirafiki tukiwa Misri, natambua kutakuwa na timu mbili za Tanzania, Simba ni timu nzuri naipa kipaumbele katika maandalizi ili kuwapa wachezaji wetu ladha ya timu inayocheza Ligi Kuu Tanzania Bara.”
Simba SC imeshacheza mchezo mmoja wa kirafiki dhidi ya Ismailia na kupata sare ya bao 1-1 mwishoni na juma lililopita, huku ikielezwa kuwa klabu hiyo huenda ikacheza mchezo mwingine wa kujipima nguvu baada ya mazoezi ya siku kadhaa zijazo.