KWA usajili ilioufanya Yanga kwa kumchukua Stephane Aziz Ki kutoka klabu ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast na Bernard Morrison wa Simba ilikuwa lazima winga Yacouba Sogne aachwe.
Yacouba anamudu zaidi kucheza kama winga na kiungo mshambuliaji nafasi ambazo inachezwa na wachezaji hao wawili ambao wametokea kuwateka mashabiki wa Yanga licha ya kwamba Ligi Kuu Bara haijaanza.
Benard Morrison licha ya kwamba msimu uliopita alikuwa hapati nafasi ya mara kwa mara ya kuanza katika kikosi cha kwanza cha Simba lakini alipokuwa akiingia uwanjani au akianza alionyesha kiwango kikubwa na zaidi aliibeba sana timu hiyo kwenye michuano ya kimataifa.
Kurejea kwa Morrison ndani ya kikosi cha Yanga kumeiweka rehani nafasi ya Yacouba na ndio maana uongozi wa klabu hiyo umefanya uamuzi mgumu wa kuachana naye.
Pia ujio wa Aziz Ki ambaye usajili wake umetikisa Tanzania nao umezidi kumpa wakati mgumu Yacouba kuendelea kusalia ndani ya Yanga kwani moja kwa moja itabidi kumpisha raia mwenzake huyo wa Burkina Faso ambaye ana nafasi ya kuingia katika kikosi cha kwanza bila shida.
ALIKWAMA HAPA
Licha ya Yacouba kuwa ni winga mzuri na ana najua sana boli, lakini majeraha ya goti yamekatisha ndoto zake za kuendelea kuichezea Yanga msimu huu.
Yacouba ndiye alikuwa kinara wa mabao ndani ya kikosi cha Yanga msimu wa 2020/21 akiifungia mabao manane na alifuatiwa na Deus Kaseke aliyefunga mabao sita.
Hata hivyo, licha ya kuanza vizuri msimu uliopita kwa kutoa pasi mbili za mabao lakini alijikuta akicheza mechi tano tu za mwanzo na baadaye kukaa nje ya uwanja msimu mzima baada ya kupata majeraha ya goti.
Mchezaji huyo alilazimika kutolewa akiwa anachechemea katika dk.31 dhidi ya Ruvu Shooting Nov.2 mwaka jana na baada ya vipimo ilionekana aliumia vibaya katika goti lake hivyo Yanga kuamua kumpeleka Tunisia kwa matibabu zaidi.
Yacouba alireja nchini Novemba 18 akitokea Tunisia baada ya kufanyiwa upasuaji uliosimamiwa na daktari bingwa Dahmane Jaleleddine ambaye amekuwa akiwatibu wachezaji wengi wa Kaskazini.
Hata hivyo, licha ya Machi mwaka huu kudai kuwa amepona na kuanza mazoezi mepesi, hakurejea uwanjani kucheza mechi yoyote na timu yake hadi sasa kukiwa na taarifa kuwa anatemwa.
Kocha mzoefu, Kenny Mwaisabula ’Mzazi’ anasema Yacouba ni mchezaji mzuri na kama Yanga wanamuacha basi itakuwa ni kwa sababu hayuko fiti.
“Yacouba uwezo wa mpira anao mkubwa tu ila kama anaachwa ni kutokana na kitabibu zadi kwani afya yake haijatengamaa hivyo viongozi wanaangalia labda huyu atachukua muda gani hadi arudi kuwa fiti.
“Kwa sasa Yanga wana mipango mikubwa ya kufanya vizuri ndani na kimataifa hivyo lazima wawe na wachezaji walio tayari kimwili na kiakili na ndio maana unaona Yacouba licha ya kwamba ni mchezaji mzuri lakini kwa sababu hayuko fiti inawaka ugumu Yanga kuendelea naye labda kama bado ana mkataba wanaweza kumpeleka sehemu kwa mkopo ili kurejesha ubora wake na baadaye wanaweza kumrudisha, anasema Mzazi.
MZIKI WA GEITA
Inadaiwa Yanga inatamani kuendelea na Yacouba kwani ni mchezaji mzuri lakini inaona kama bado hayuko fiti kuitumikia timu hiyo kwa sasa huku pia ikimtema straika Chico Ushindi.
Uwepo wa wachezaji wengi wa kimataifa katika kikosi cha Yanga ndio uliwapa wakati mgumu viongozi wa klabu hiyo kuamua nani abaki na nani aachwe lakini ilibidi wafanye uamuzi mgumu tu wa kumtema Yacouba na Chico.
Taarifa zilizopo ni kwamba Yanga wako katika mzungumzo na Yacouba pamoja na klabu ya Geita ili mchezaji huyo aende kukitumia kikosi hicho msimu ujao.
Yanga inasubiri kuona kama Yacouba atakubali jambo hilo au atakataa na kuamua kutimka kabisa nchini.
Yanga inatamani Yacouba achezee Geita ili baadaye kama akirudi katika ubora wake wamsajili tena kwani bado wanaamini ni bonge la mchezaji lakini majeraha tu ndiyo yameshusha kiwango chake.
Mwenyekiti wa Bodi ya Geita Gold, Constantine Morandi alisema suala la kumalizana na Yacouba lipo kwenye hatua nzuri huku akithibitisha mazungumzo ya mchezaji huyo ni baina yao na Yanga.
“Tulishapeleka barua ya kumuomba Yacouba na tuliambiwa tusubiri atakaporejea kutoka mapumzikoni ili tuweze kumalizana nao nadhani kama mlivyosikia Yanga wakisema kuna mazungumzo basi ni baina yetu sisi Geita, mchezaji mwenyewe na waajiri wake wa zamani Yanga,” anasema Morandi.