Mabosi wa Singida Big Stars umemwongezea mkataba wa miaka miwili kiungo, James Kotei kwa ajili ya kuendelea kuichezea msimu ujao.
Taarifa zinadai nyota huyo alianza mazungumzo na klabu nyingine baada ya kurejea kwao Ghana wakati huo akiwa kipindi cha mapumziko ila uongozi wa Singida uliposikia habari hizo wakafanya mawasiliano ya haraka na kumrudisha nchini.
“Amerudi na ameanza mazoezi na wenzake, ni mchezaji mzuri ambaye alitusaidia hadi tunapanda ligi kuu hivyo tuliona ni vizuri kumshawishi tukiamini uzoefu wake utaleta manufaa kwenye kikosi chetu,” kilisema chanzo hicho.
Akizungumzia hilo, Kotei alisema amefurahia kurejea tena Tanzania akiamini ni sehemu nzuri na yenye ligi ya ushindani.
“Nimefurahi kuungana na Said Ndemla kwenye kikosi chetu baada ya awali kucheza naye tukiwa Simba, tumeishi kama ndugu kwa kipindi kirefu na kucheza tena pamoja naamini tutafanya makubwa msimu ujao,” alisema Kotei.
Kotei aliyeichezea Simba kwa misimu miwili kuanzia 2017-2019 alitua nchini juzi kukamilisha dili hilo kisha kuungana moja kwa moja na kikosi hicho jijini Arusha kilichoweka kambi ya kujiandaa na maandalizi ya msimu (pre season).