Nguvu ya fedha baina ya matajiri watatu wanaozipa nguvu ya kiuchumi Simba, Yanga na Azam huenda ikawa na mchango mkubwa katika kuamua vita ya kuwania mataji baina ya timu hizo.
Mabilionea hao ni Mohamed Dewji upande wa Simba, Gharib Said Mohamed (GSM) kwa Yanga pamoja na Yusuf Bakhresa (Azam).
Kujitosa kwa mtoto wa bilionea Said Bakhresa, Yusuf Bakhresa katika kuisimamia Azam FC hapana shaka kunawapa kibarua kigumu Dewji na GSM ambao katika misimu ya hivi karibuni jeuri yao ya fedha imekuwa chachu kwa Simba na Yanga kufanya vizuri hapa nchini.
Awali, Azam FC ilionekana kuacha shughuli nyingi za uendeshaji na usimamizi mikononi mwa ofisi ya mtendaji mkuu, Abdulkarim Amin ‘Popat’ lakini sasa mambo yamekuwa kinyume ambapo Yusuf Bakhresa ameamua kushiriki moja kwa moja jambo linaloonyesha amepania vilivyo kusaka heshima mbele ya GSM na MO Dewji.
Kutokana na hilo, ni wazi kwamba kuanzia msimu ujao wa Ligi, Azam inaongezeka kama timu ya tatu kwenye kinyang’anyiro cha mataji mawili makubwa nchini ya Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho la Azam.
Licha ya Yanga, Azam na Simba kuwa na wadhamini ambao wanazipa fedha kwa ajili ya kujiendesha, hapana shaka yoyote mchango wa Yusuf Bakhresa, MO Dewji na Gharib kiuchumi ndio kwa kiasi kikubwa utaamua vita ya ubingwa msimu ujao.
USAJILI
Kabla hata ya msimu kuanza, matajiri hao watatu kila mmoja ameshaonyesha jeuri ya fedha kwa kutoa fungu nono la usajili kwa timu yake kwa ajili ya kunasa vifaa vya kuimarisha kikosi cha kila upande.
Hadi sasa kila bilionea inakadiriwa amemwaga zaidi ya Sh 1 bilioni ili kufanikisha mchakato wa usajili katika timu yake jambo ambalo linaashiria wazi, msimu ujao patachimbika.
Wakati GSM akitoa mpunga huo kuwanasa Stephane Aziz Ki, Joyce Lomalisa, Gael Bigirimana, Lazarous Kambole na Bernard Morrison.
Yusuf Bakhresa yeye amewasajili wachezaji tisa ambao ni Tape Edinho, Kipre Junior, James Akaminko, Abdul Sopu, Nathaniel Chilambo, Malickou Ndoye, Cleoface Mkandala, Isah Ndala na Ali Ahamada.
Kwa upande wa Dewji, mzigo wake umefanikisha usajili wa Augustine Okrah, Nelson Okwa, Mohamed Ouattara, Victor Akpan, Habib Kyombo, Moses Phiri na Nassoro Kapama, huku dili la straika Cesar Manzoki, likipata vikwazo kutoka klabu yake ya Vipers ya Uganda.
MAANDALIZI YA MSIMU
Kambi za kifahari ambazo timu hizo zimeweka kujiandaa na msimu ujao ni matokeo ya jeuri ya fedha ambayo kila moja inapata kutoka kwa bilionea ambaye yupo juu yake.
Wakati Yanga wakiweka kambi katika eneo la kifahari la Avic Town, Kigamboni, Dar es Salaam, Simba na Azam FC zenyewe zimekimbilia huko Misri katika miji tofauti.
Simba wao wameweka kambi yao katika Jiji la Ismailia huku Azam FC wenyewe wakijichimbia huko El Gouna.
POSHO, BONASI, MISHAHARA
Mbali na kushiriki katika usajili na kugharamia kambi za maandalizi ya msimu, mabilionea hao pia watagharamia kiasi fulani cha fedha katika bajeti ya mishahara ya nyota wa vikosi vyao lakini pia posho.
Lakini imejengeka utamaduni kwao kutoa bonasi kwa timu zao pindi zinapofanya vizuri katika mechi za mashindano ya ndani na nje.
Wenyewe wafunguka.
Mara baada ya kufanya usajili wa kishindo, Yusuph Bakhresa amewaambia mashabiki wa timu hiyo kukaa mkao wa kula huku akiwataka waisapoti katika mashindano yaliyo mbele yao.
“Nawaahidi furaha zaidi msimu ujao, mashabiki wa Azam FC na wa soka kiujumla. Nawaomba mzidi kuiunga mkono timu yenu msimu ujao. Tukutane msimu ujao,” alisema Bakhresa.
Kwa upande wake mwekezaji wa Simba, Dewji alisema baada ya kutofanya vizuri msimu uliopita, wamejipanga kurudi upya msimu ujao.
“Hakuna kurudi nyuma. Tunatakiwa kufanya mabadiliko katika maeneo ambayo tuna upungufu na kwenda mbele. Mapambano yanaendelea wala hakuna kukata tamaa,” alisema Dewji.