Home Habari za michezo ‘PROFESA’ NABI AZIDI KUIWEKA NJIA PANDA YANGA…MKATABA WAKE WAENDELEA KUZUNGUKA TAREHE…

‘PROFESA’ NABI AZIDI KUIWEKA NJIA PANDA YANGA…MKATABA WAKE WAENDELEA KUZUNGUKA TAREHE…


WAKATI programu ya Kocha wa Yanga, Nesreddine Nabi, kucheza mechi za kirafiki itaanza wiki ijayo, huku timu hiyo ikijifua saa tano kwa siku sawa na dakika 300, mazungumzo yanaendelea kuhusu mkataba wake mpya na kila kitu kitawekwa wazi muda si mrefu kwa muda gani ambao ameongeza.

Kikosi cha Yanga kilianza mazoezi rasmi wiki iliyopita kwa kufanya mazoezi mara moja ya uwanjani na sasa wanafanya mazoezi mara mbili kwa siku asubuhi na jioni.

Asubuhi wanafanya saa mbili na jioni saa tatu na kutimiza jumla ya saa tano sawa na dakika 300 kwa siku.

 Nabi alisema kwa sasa wanaendelea kufanya mazoezi ya Gym kwa ajili ya viungo ambayo yanafanyika asubuhi na jioni uwanjani kwa ajili ya kuweka fiti wachezaji wake.

Alisema ameridhishwa na maendeleo ya kikosi chake na kutarajia makubwa zaidi kwa sababu wachezaji hao wamerejea wakiwa vizuri katika suala la utimamu wa mwili.

“Mechi za kirafiki bado kwa sasa kwa sababu wiki hii tunaendelea na program ya mazoezi, nina imani mwishoni mwa wiki hii au mwanzoni mwa wiki ijayo tutaanza kucheza mechi za kirafiki kwa ajili ya kujipima,” alisema Nabi.

Alisema maandalizi yanaenda vizuri na wachezaji wanaelewa kile anachofundisha na kutarajia makubwa zaidi wachezaji wote watakapowasili kambini.

Ofisa habari wa klabu hiyo, Hassan Bumbuli alisema wachezaji wa kigeni wawili, Bernard Morrison na Yannick Bangala wameingia jana na leo wataungana na wenzao mazoezini kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya.

“Wachezaji wote (wazawa) ambao hawako katika majukumu ya timu ya Taifa, wako kambini na wakigeni kasoro hao wawili ambao wanarejea leo (jana) na kesho (leo) wataingia kambini kuanza rasmi msimu mpya wa ligi,” alisema Bumbuli.

Alisema kuhusu mkataba wa kocha wa Nabi, mazungumzo yanaendelea na wiki ijayo kila kitu kitawekwa wazi ikiwemo ni muda gani wa mkataba ambao ameongeza.

“Kikubwa ni kwamba Nabi amethibitisha kuendelea na Yanga na sasa yuko katika maandalizi ya msimu mpya nadhani juu ya mkataba wake tutaweka wazi hili linafanyika sambamba na suala la Yacouba Sogne juu ya makubaliano yetu kwa sababu tayari amemaliza mkataba,” alisema Bumbuli.

SOMA NA HII  SIKU CHACHE BAADA YA KUULA TENA SIMBA....KABURU AIBUKA NA NENO HILI KWA MO DEWJI...

Alisema ndani ya wiki hii watakuwa na jambo lao ikiwemo kumtangaza rasmi mdhamini wao Mkuu ambaye ameweka mamilioni ya fedha katika klabu hiyo.

Bumbuli alisema mbali na kuweka wazi udhamini huo lakini pia watazindua rasmi siku ya Wananchi, kuweka wazi mgeni rasmi na timu watakayocheza nayo siku ya kilele, Agosti 6, mwaka huu kabla ya kuanza mchezo wa ufunguzi wa ligi.

Yanga wanaendelea kujifua katika kambi yao ya Avic Town, Kigamboni kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya, lakini wakikumbuka Agosti 13, watakuwa na kibarua pevu kuwakabili Simba na mchezo wa Ngao ya Jamii.