Home Habari za michezo KWA YANGA HII YA MAYELE, AZIZI KI NA MORRISON…UKIPONA SAANA BASI UJUE...

KWA YANGA HII YA MAYELE, AZIZI KI NA MORRISON…UKIPONA SAANA BASI UJUE GOLI TATU AU NNE ZINAKUHUSU…


FISTON Mayele amemaliza utata kwa kukubali kusaini mkataba mpya wa mwaka mmoja na sasa atakuwa kikosini hadi 2024, lakini usajili wa Stephane Aziz KI na Bernard Morrison ‘BM33’ umewafanya wakongwe kushindwa kujizuia wakisema sasa jamaa atafunga sana.

Msimu uliopita Mayele alimaliza kinara wa mabao wa timu hiyo akifunga mabao 16 nyuma ya George Mpole wa Geita Gold aliyebeba tuzo ya Mfungaji Bora wa Ligi Kuu, huku mengi yakitokana na asisti za mabeki, kitu ambacho inaelezwa safari hii atapata ahueni kwa kina BM33.

Mayele alibakiza mkataba wa mwaka mmoja kati ya miwili aliyoingia na Yanga msimu uliopita na inaelezwa amekubali kuongeza mwaka kusalia kikosini baada ya kufanya kikao na bilionea Ghalib Said ‘GSM’ ikiwemo kuboreshewa mshahara na marupurupu mengine.

Kama mambo yataenda vizuri maana yake ataendelea kuwa straika namba moja, huku nyuma na pembeni yake watakuwapo Aziz KI na BM33 wanaotajwa wamekuja kumrahisishia kazi ya kufunga tofauti na ilivyokuwa msimu uliopita.

Kuanza kikosini kwa Aziz Ki na BM33 kunawapa matumaini makubwa mastaa wa zamani na mashabiki wa Yanga, akiwamo Abedi Mziba ‘Tekero’ wakiamini kutaongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji ambayo msimu uliopita ilimaliza na mabao 49 katika mechi 30.

Hata hivyo, uwepo wa nyota hao unaweza kufurahiwa zaidi na Mayele pengine kuliko mchezaji mwingine kikosini kutokana na uwezo mkubwa wa kupiga pasi za mwisho ambao unaweza kuwa faida kwa mshambuliaji huyo kutoka DR Congo.

Yanga sasa ina uhakika wa kutengeneza idadi kubwa za nafasi jirani na eneo la timu pinzani zinazoweza kuwa na faida kwa Mayele tofauti na msimu uliopita ambao licha ya kufunga mabao 16 Ligi Kuu hakupata huduma ya kutosha kutoka kwa viungo washambuliaji.

Takwimu za msimu uliopita zinaonyesha idadi kubwa ya mabao ya Mayele yalitokana na mchango wa wachezaji wa nafasi ya ulinzi, huku machache ya viungo washambuliaji tatizo ambalo Aziz Ki na Morrison wana kibarua cha kulitibu.

SOMA NA HII  AFISA HABARI SIMBA AFUNGUKA ISHU YA YANGA KUMTAKA AENDE KWAO...AGUSI ISHU YA KUFUKUA MAFAILI...

Kati ya mabao 16 ambayo Mayele alifunga manane yalitokana na pasi za mwisho za mabeki, matano kutoka kwa viungo washambuliaji na moja likifungwa na kiungo wa kati huku mengine yakitokana na makosa ya mabeki wa timu pinzani.

Djuma Shaban ambaye ni beki wa kulia ndiye alikuwa kinara wa kumlisha Mayele pasi za mabao ambapo alimuasisti mara tano akifuatiwa na kiungo mshambuliaji, Saido Ntibazonkiza aliyeasisti mara tatu kwa Mayele.

Asisti nyingine za Mayele zilitoka kwa kiungo mshambuliaji Feisal Salum ‘Fei Toto’ na beki wa kushoto, Yassin Mustafa kila mmoja alimpa mbili huku beki kiraka Kibwana Shomari na kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ kila mmoja akipiga pasi moja ya mwisho.

Katika msimu uliomalizika Morrison na Aziz Ki walikuwa na takwimu bora za kupiga pasi za mwisho kuliko kiungo yeyote wa ushambuliaji Yanga kwenye mashindano mbalimbali.

Morrison ambaye alikuwa Simba alikuwa na pasi za mwisho sita ambapo tano zilikuwa za klabu Afrika na moja Ligi Kuu wakati Aziz Ki kwenye mechi 26 za mashindano alizoichezea Asec Mimosas alipiga pasi za mwisho nne.