Home Azam FC BAADA YA KUTUA AZAM FC…..SOPU AVUNJA UKIMYA…AFUNGUKA NAMNA ISHU NZIMA ILIVYOKUWA…

BAADA YA KUTUA AZAM FC…..SOPU AVUNJA UKIMYA…AFUNGUKA NAMNA ISHU NZIMA ILIVYOKUWA…


Mshambuliaji na mfungaji bora wa Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), Abdul Suleiman ‘Sopu’ ameonyesha kuwa na mzuka wa kuanza maisha yake mapya kwenye klabu ya Azam ambapo ametamka kuwa mashabiki na viongozi timu hiyo wategemee makubwa kutoka kwake.

Usiku wa Alhamisi, Sopu alitwaa tuzo tatu zilizotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ikiwa ni siku chache baada ya pazia la Ligi Kuu Bara kufungwa pamoja na fainali ya ASFC kati ya Coastal Union dhidi ya Yanga.

Tuzo hizo ni mchezaji na mfungaji bora akiwa na mabao tisa kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC) na tuzo ya tatu ni ile ya kikosi bora cha Ligi Kuu Bara.

Sopu alitisha katika michuano ya ASFC ambako aliandika historia mpya baada ya kupachika mabao matatu kwenye mchezo wa fainali ambao Coastal Union ilipoteza kwa penalti 4-1 baada ya dakika 120 za pambano kumalizika kwa sare ya mabao 3-3.

Sopu ambaye amesaini mkataba wa miaka mitatu Azam FC akitia kibindoni mkwanja wa maana unaotajwa kuwa ni Sh100 milioni, alisema anatambua ukubwa wa timu hiyo lakini kwa kiasi fulani ana uzoefu wa kucheza kwenye timu kubwa kwani aliwahi kuitumikia Simba miaka ya nyuma.

“Presha kwa mchezaji ni jambo la kawaida na muda mwingine huwa chachu kwa mchezaji kufanya vizuri, hata Coastal kuna muda wachezaji tulikuwa tukikumbana na presha kwa sababu timu ilikuwa ikihitaji kumaliza msimu vizuri,” alisema na kuongea:

“Natambua Azam ni timu kubwa na nisingependa kuwa mzungumzaji sana lakini ahadi yangu ni kutoa mchango wangu kwa asilimia 100 kama ilivyokuwa Coastal ili kufanikisha malengo ya timu na kuwafurahisha mashabiki.”

Sopu anaonekana kuwa na uzoefu mkubwa wa kucheza Ligi Kuu Bara licha ya kuwa na umri mdogo, inakumbukwa kuwa aliwahi kufanya vizuri akiwa na Ndanda kabla ya kutua Simba ambako alishindwa kucheza kikosi cha kwanza ndipo alitimkia Coastal Union inayonolewa na Juma Mgunda.

SOMA NA HII  MAAFISA CAF KUTEMBELEA UWANJA WA MKAPA KUONA KAMA 'YALIYOMO YAMO AU LAAH'..FAINAL ITAPIGWA...

Upande wa Mgunda ambaye anaamini kuwa Sopu ndiye mchezaji wake bora msimu wa 2021/22 licha ya usiku wa tuzo kutangazwa Yannick Bangala wa Yanga, alisema amezungumza na mchezaji wake na kumshauri mambo ya kuzingatia ili aendelee kufanya vizuri.

“Huyu ni kijana wangu hivyo nimekaa naye chini na kumweleza mambo ya msingi ambayo anapaswa kuyashika, anaweza kuendelea kufanya vizuri akiwa Azam, kiukweli nimemtakia kila la kheri,” alisema kocha huyo.

Mgunda alianza kumnoa Sopu timu ya taifa ya Tanzania ya vijana wa umri chini ya miaka 20 ‘Ngorongoro Heroes’ kabla ya kuungana Coastal.

Sopu ametabiriwa kufika mbali kama ataongeza juhudi kutokana na mwendelezo kupaji chake akionekana kukua kila mwaka. Msimu uliopita alishinda tuzo ya Mchezaji Chipukizi Bora kabla ya msimu huu kutisha zaidi.